Kinda JKT Queens azungumzia ushindani wa namba

KIUNGO fundi wa JKT Queens, Elizabeth John amesema ushindani wa namba katika kikosi hicho ni mkubwa hasa eneo la kiungo, lakini umechangia kuongeza kiwango cha wachezaji.

Huu ni msimu wa pili nyota huyo wa zamani wa Alliance Girls kuitumikia JKT, msimu uliopita alikuwa mbadala wa Joyce Lema aliyekuwa nje msimu mzima akiuguza majeraha.

Elizabeth ambaye ni mmoja wa chipukizi wanaopata nafasi kikosini humo, amesema kila mchezaji anaonyesha bidii mazoezini ili kujihakikishia nafasi ya kucheza.

“Ushindani wa namba ni mkubwa sana, kila  mchezaji yupo tayari kupigania nafasi yake, kila anayeonyesha mazoezini anapata nafasi ya kuanza na binafsi napambana ili nimwonyeshe kocha naihitaji,” amesema Elizabeth.

Aliongeza uwepo wa wachezaji wenye uzoefu katika kikosi hicho umemsaidia kujifunza haraka, hasa katika maamuzi ya ndani ya uwanja na kuongeza kujiamini anapopewa nafasi ya kucheza.

“Kucheza na wachezaji wakubwa kama Donisia Minja kunanisaidia sana, wanatupa ushauri, wanatuelekeza na hilo linatupa motisha sisi vijana kuendelea kupambana,” aliongeza.

Kwenye eneo la kiungo wapo nyota kama Minja, Lema, Janeth Pangamwene ambao wamekuwa wakipata nafasi na kuanza kikosini hapo.

Msimu huu kinda huyo hadi sasa amecheza mechi nne kati ya nane za JKT.