KASI ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka nje kurudi nyumbani inazidi kuongezeka baada ya kiungo mshambuliaji wa zamani wa Beykoz Anadolu Spor ya Uturuki, Shafii Omary Kimambo naye kuunga juhudi akipewa mkataba wa miaka miwili klabu ya Ligi Kuu Bara, KMC.
Kinda huyo wa miaka 20 hii inakuwa timu ya kwanza ya Ligi Kuu kuitumikia na aliwahi kukipiga Tuzlaspor ya Uturuki.
Mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti, tayari KMC wamemalizana na kiungo huyo na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa kikosini hapo.
Aliongeza sababu ya kurejea Tanzania ni pamoja na changamoto alizokutana nazo nje ya uwezo wake ambazo viongozi wa timu hiyo walishindwa kuzitatua.
“Amesaini Ijumaa mkataba wa miaka miwili kila kitu tayari na kuanzia sasa wanaweza kumtambulisha, kuna vitu vilikuwa vinakwamisha kule Uturuki akaamua kurejea Tanzania lakini kuna timu nyingi zilikuwa zinahitaji huduma yake,” amesema mtu huyo na kuongeza
“Dili lilimalizwa na kocha wa sasa wa KMC, Mohamed Baresi ambaye anamfahamu hivyo akawaambia viongozi anamhitaji alipoletewa ofa yao akaona inafaa ndipo akasaini.”
KMC iko mkiani mwa msimamo wa ligi kwenye mechi tisa imeshinda moja, sare moja na kupoteza saba ikikusanya pointi nne.
Shafii anaunga tela la wachezaji wa Kitanzania waliokuwa wakicheza nje ya nchi waliorejea nchini akiwamo mkongwe Himid Mao, Yahya Zayd, Muhsin Malima na Adolf Mtasingwa waliopo Azam FC, Nickson Kibabage aliyetua Simba akitokea Singida BS, Shaaban Idd Chilunda, Farid Mussa, Abdi Banda, Morice Abraham, Mwanahamis Omar ‘Gaucho na wengineo.