Kufukuliwa mto Delhu kwarejesha tabasamu

Moshi. Wananchi wa maeneo ya Kisangesangeni na Mauru, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameeleza matumaini mapya ya kuondokana na adha ya mafuriko pamoja na upungufu wa maji ya umwagiliaji, kufuatia kuanza kwa kazi ya kufukua na kuongeza kina cha maji katika Mto Delhu na kuurejesha katika mkondo wake wa asili.

Kazi hiyo inatekelezwa na wataalamu kutoka Bonde la Maji la Pangani, ikiwa na lengo la kudhibiti mafuriko, kulinda makazi na mashamba ya wananchi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Wakizungumza leo kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema mto huo ulikuwa umejifukia kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 hadi 20, hali iliyosababisha mafuriko makubwa kila msimu wa mvua na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi baada ya kuharibu makazi na mashamba yao.

Mkazi wa Kisangesangeni, Michael Kitali, amesema kila msimu wa mvua kuanzia Machi hadi Juni, wananchi walikuwa wakiishi kwa hofu kubwa kutokana na maji yanayotoka ukanda wa milimani kusambaa kwenye makazi na mashamba ya wananchi.

“Mafuriko haya hayakusababishwa na mvua zinazonyesha huku, bali zile za milimani. Mto ulikuwa umejaa tope na kupoteza kina chake hivyo maji yalikuwa yakisambaa. Hali hii ilitudhoofisha kiuchumi kwani tulishindwa kulima kipindi cha mvua,” amesema Kitali.

Kwa upande wake, Miriam Mdee amesema mafuriko yalikuwa yakiathiri maisha ya kila siku, hususan elimu ya watoto na usalama wa familia.

“Kipindi cha mvua watoto walishindwa kwenda shule, maji yaliingia ndani ya nyumba na kuharibu mashamba. Lakini sasa mto umeongezewa kina na kupanuliwa, maji yatapita mtoni na hayatatusumbua tena,” amesema.

Naye Monica Said, mkazi wa Mauru, amesema mafuriko yalikuwa kikwazo kikubwa kwa kina mama, wajasiriamali na wagonjwa.

“Tulishindwa kwenda sokoni, kuvusha watoto kwenda shule na hata kufika hospitali. Wengine tuliogopa kubeba mimba kwa hofu ya kushindwa kufika kliniki kipindi cha mvua. Kupanuliwa kwa mto huu ni neema kubwa kwetu,” amesema Monica, akishukuru Serikali kwa hatua hiyo.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Skimu ya Umwagiliaji Kimwangamao, Petet Kessy, amesema mafuriko na kujaa kwa tope kwa Mto Dehu kulisababisha upungufu mkubwa wa maji ya umwagiliaji, hasa pale wakulima wa maeneo ya juu walipofungua maji.

Kessy amesema kurejeshwa kwa mto katika mkondo wake wa asili na kuongezwa kina kutapunguza migogoro ya maji na kuhakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika katika Skimu ya Kimwangamao inayohudumia mashamba yenye ukubwa wa hekta 5,600.

“Ukuta unaojengwa pembezoni mwa mto utapunguza mafuriko, na kwa kuwa mto sasa unapitisha maji vizuri, hata mvua zikinyesha maji hayatatawanyika tena kwenye makazi ya wananchi,” amesema Kessy.

Kwa upande wake Innocent Thadeo, Mtaalamu wa Maji Juu ya Ardhi kutoka Bonde la Maji Pangani, amesema lengo la kufukua mto ni  kuongeza kina cha maji, kupanua mkondo na kuweka matuta ili kuzuia athari za mafuriko, huku mto ukirejeshwa katika sehemu yake ya asili ili wananchi wanufaike na rasilimali hiyo.

Ameongeza kuwa kurejeshwa kwa mto kutasaidia pia upatikanaji wa maji ya umwagiliaji katika Skimu ya Kimwangamao, na Bonde la Maji Pangani limeendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi karibu na mito juu ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali maji ili kuzuia changamoto hiyo kujirudia.