Dar es Salaam. Kadri gharama za maisha zinavyozidi kupanda na mfumuko wa bei kuendelea kuathiri thamani ya fedha, wataalamu wa uchumi na masuala ya kifedha wanawashauri Watanzania kubadili mtazamo wao kuhusu biashara na uwekezaji.
Wanasema, katika mazingira ya sasa ya kiuchumi, uwekezaji si tena fursa ya matajiri pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kujenga usalama wa kifedha hata kwa watu wenye kipato cha kawaida.
Katika hali ya sintofahamu inayosababishwa na utegemezi wa mishahara isiyokidhi mahitaji na akiba isiyozaa faida, wataalamu wanashauri Watanzania kutafuta njia mbadala za kuwekeza kwa busara ili kujihakikishia faida na uthabiti wa kifedha wa muda mrefu.
Kwa mujibu wa wachambuzi, mazingira ya kiuchumi ya Tanzania bado yanatoa fursa nyingi za uwekezaji kutokana na ukuaji endelevu wa uchumi na uimara wa mifumo ya masoko ya kifedha.
Wanasema uwekezaji si fursa ya watu wenye mitaji mikubwa pekee, bali ni nyenzo muhimu hata kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati, mradi kuwepo nidhamu ya matumizi, maarifa ya kifedha na uvumilivu huku wakiainisha maeneo ambayo mwenye kipato cha kawaida anaweza kuwekeza.
Maeneo hayo ni pamoja na kwenye mali zisizohamishika, kilimo cha kibiashara, ununuzi wa hati fungani na hisa, biashara za aina mbalimbali, mifuko ya uwekezaji, sekta ya utalii na utoaji huduma.
Hata hivyo, Dk Adam Kalinga, mchambuzi wa masuala ya uchumi, amesema changamoto kubwa kwa Watanzania wengi si kukosa kipato, bali kukosa mkakati wa kukilinda dhidi ya kushuka kwa thamani ya fedha.
“Fedha inayohifadhiwa bila kuwekewa mkakati wa uwekezaji inapoteza thamani kila mwaka. Ndiyo maana uwekezaji leo si jambo la hiari, ni hitaji la lazima,” amesema.
Amesema uwekezaji unapaswa kuzingatia malengo ya mtu, muda alionao na kiwango cha hatari anachoweza kustahimili.
Sekta ya mali isiyohamishika ikihusisha ardhi na majengo inaendelea kuongoza kwa kuaminika kwa wananchi wengi, hasa kutokana na ongezeko la watu mijini na upanuzi wa miji kama Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Mwanza.
Ili kupata manufaa ya uwekezaji huo, Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Joseph Mrema, amesema: Huna haja ya kuanza na nyumba ya gharama kubwa. Kiwanja katika eneo linalokua au nyumba ndogo ya vyumba viwili kwa ajili ya kupanga ni mwanzo mzuri,” amesema.
Ameeleza ardhi na majengo huongezeka thamani kwa muda na pia huweza kumletea mmiliki mapato ya uhakika kupitia kodi.
Kwa mtazamo wa Abdul Said, dereva wa teksi mkazi wa Temeke, uwekezaji katika mali isiyohamishika unaonekana mzuri lakini ni changamoto kwa wenye kipato cha chini.
“Kiwanja hata cha mbali, kinahitaji fedha na uvumilivu. Hata hivyo, wazo la kuanza hatua ndogo limenipa matumaini kwamba hata sisi tunaweza kufika huko taratibu,” amesema.
Licha ya hofu iliyokuwepo kwa muda mrefu, wataalamu wa masoko ya fedha wanasema uwekezaji katika hisa ni fursa isiyopaswa kupewa kisogo na Watanzania, kwa mujibu wa Asha Msuya, mchambuzi wa masoko ya mitaji.
Amesema soko la hisa Dar es Salaam (DSE) ambalo mtaji wake umeshuhudia ukuaji mkubwa siku za hivi karibuni, limeendelea kurahisisha ushiriki wa wawekezaji wadogo.
“Kununua hisa ni kumiliki sehemu ya kampuni. Unapata faida kampuni inapokua kupitia gawio au kupanda kwa thamani ya hisa zako,” anasema.
Ameshauri wawekezaji wapya kuanza kwa kiasi kidogo, kuchagua kampuni zenye rekodi nzuri na kuepuka kuingia sokoni kwa tamaa ya faida ya haraka.
Kwa wale wasiopenda hatari kubwa, hati fungani za Serikali zinatajwa kama uwekezaji salama kama anavyofafanua mhadhiri wa masuala ya fedha, Dk Emanuel Nnko, kuwa uwekezaji huu unawafaa zaidi waajiriwa na watu wanaotafuta mapato thabiti.
“Unapoziweka fedha zako kwenye hati fungani, unaiamini Serikali. Riba hulipwa kwa uhakika na mtaji wako unalindwa. Hata mwenye kipato cha kawaida anaweza kuanza kuwekeza kupitia benki au madalali waliothibitishwa,” amesema.
Mbali na hati fungani za Serikali, zipo za manispaa na za kampuni binafsi, ambazo kwa wastani zote hutoa faida ya zaidi ya asilimia 12 kwa mwaka.
Biashara ndogo na za kati zinaendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa Watanzania wengi na changamoto yao kubwa si kukosa wateja bali ni usimamizi duni wa fedha.
“Biashara nyingi zinaanguka kwa sababu mapato ya biashara yanachanganywa na matumizi binafsi. Nidhamu ya kifedha ndiyo msingi wa mafanikio,” amesema Paul Kweka ambaye ni mshauri wa biashara.
Amesema biashara za chakula, huduma, usafiri, pamoja na biashara ndogo za teknolojia zinaendelea kuwa na mahitaji makubwa, hasa mijini.
Wataalamu wa uchumi wamesema sekta ya kilimo bado ina fursa kubwa kwa wawekezaji wa kipato cha kawaida, iwapo itafanywa kwa mtazamo wa kibiashara.
Rehema Msuya ambaye ni mtaalamu wa uchumi amesema kilimo cha mazao yenye mzunguko mfupi wa fedha kinaweza kumletea mkulima faida kwa haraka.
“Mazao ya mbogamboga, matunda, ufugaji wa kuku au samaki yana soko la uhakika. Kilimo kikifanywa kwa kuzingatia soko, kina faida kubwa,” amesema na kuongeza kuwa usindikaji wa mazao huongeza thamani na kipato kwa mkulima.
Kwa Watanzania wanaofanya kazi za kuajiriwa au wasiokuwa na muda wa kusimamia biashara, mifuko ya uwekezaji wa pamoja inatajwa kuwa mbadala salama, kulingana na ushauri wa Grace Lema, mchambuzi wa masuala ya fedha.
Amesema mifuko ya uwekezaji kama UTT na mingine inamwezesha mtu kuwekeza hata kwa kiasi kidogo ambapo fedha zinakusanywa na kuwekezwa na wataalamu na hivyo kupunguza hatari na kumwondolea mwekezaji mzigo wa usimamizi,” amesema.
Eneo jingine ni utalii na huduma ndogo ndogo ambazo ni fursa kwa wawekezaji wadogo kupitia nyumba za kulala wageni, migahawa midogo na biashara za bidhaa za utalii.
Wataalamu wanasema ukuaji wa utalii wa ndani umeongeza mahitaji ya huduma hizo, hasa katika miji na maeneo yenye vivutio vya asili.
Mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam, Juma Ally amesema kwa muda mrefu amekuwa akiweka akiba benki bila mpango wowote wa uwekezaji kwa sababu hana elimu hiyo.
“Nilikuwa na hofu kuwekeza kwa sababu ya kipato changu kuwa cha kawaida. Lakini nimekuwa nikisikia kuhusu hati fungani na baadhi ya watu ninaowajua wamenufaika, hii imeanza kunipa ujasiri nafikiria na mimi kuwekeza huko,”
Kwa upande wake Rehema Kessy ambaye ni mamalishe, amesema anafahamu umuhimu wa uwekezaji lakini changamoto kubwa kwake imekuwa ni kuchanganya fedha za biashara na matumizi binafsi.
“Ukweli ni kwamba biashara ndogo zinaweza kukuza kipato, lakini bila nidhamu ya fedha unajikuta unapiga hatua moja mbele na mbili nyuma. Ushauri wa wataalamu unaonyesha wazi wapi tumekuwa tukikosea,” amesema.
Lakini, Mariam Selemani yeye amesema watu wengi wanashindwa kuwekeza kutokana na kukosa elimu ya fedha.
“Tumekuwa tukisikia watu wakipoteza fedha kwenye miradi hewa kwa sababu ya kukimbilia faida ya haraka. Ushauri wa kuwekeza kwa mchanganyiko na kwa uvumilivu ni muhimu sana,” amesema.
Hata hivyo wataalamu wamesema hatua ya kwanza kabla ya kufanya uwekezaji katika eneo fulani, mhusika anapaswa kubadili mtazamo na kutambua kuwa uwekezaji ni safari, si tukio la siku moja.
Akizungumzia hilo, Kweka amesema kuanza mapema, hata kwa kiasi kidogo, humsaidia mtu kujenga nidhamu na kuzoea utamaduni wa kuwekeza.
Sambamba na hilo amesisitiza umuhimu wa elimu ya kifedha kabla ya kuwekeza na watambue kuwa uvumilivu ni msingi wa mafanikio ya uwekezaji.
“Kujifunza, kuuliza na kushauriana na wataalamu na waliokutangulia husaidia kuepuka maamuzi ya pupa yanayoweza kuleta hasara. Kitu kingine muhimu epuka kuweka fedha zote katika eneo moja.
“Uwekezaji mchanganyiko husaidia kupunguza hatari pale sekta moja inapopata changamoto. Faida ya kweli huonekana kwa muda mrefu, si mara moja,” amesema Kweka.