BAADA ya Mbeya Kwanza kumuuza, Boniface Mwanjonde aliyejiunga na Fountain Gate dirisha hili dogo la Januari 2026, mabosi wa kikosi hicho wamekamilisha usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wa maafande wa Tanzania Prisons, Lucas Sendama.
Sendama ameenda kuzipa nafasi ya aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Mwanjonde, ambaye ameondoka, huku akiwa amehusika kwenye mabao 13, katika mechi 14, alizoichezea Mbeya Kwanza, baada ya kufunga tisa na kuasisti mengine manne.
Mshambuliaji huyo aliyezichezea pia KenGold, Geita Gold, Biashara United na DTB iliyobadilishwa jina baadaye na kuitwa Singida Big Stars baada ya kupanda Ligi Kuu Bara, alijiunga na Prisons Agosti 14, 2025, baada ya kuondoka Stand United.
Msimu wa 2024-2025, Sendama aliifungia Stand mabao manne Ligi ya Championship na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu na pointi 61, jambo lililosababisha kucheza mechi za (Play-Off) kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara na kukwama.
Stand ilicheza mtoano na Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56 na kuiondosha kwa kuichapa jumla ya mabao 4-2, kisha hatua iliyofuata ikakutana na Fountain Gate iliyotolewa na Tanzania Prisons na kikosi hicho kuchapwa jumla ya mabao 5-1.