Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikitimiza miaka 33 tangu kuanzishwa kwake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa chama hicho (Bazecha), Suzan Lyimo amesema kuwanyima wanawake nafasi za juu za uteuzi ni miongoni mwa changamoto sugu inayoendelea kukikabili chama hicho.
Lyimo amesema nyadhifa za juu za uteuzi ambazo ni Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, hazijawahi kushikwa na mwanamke tangu chama hicho kilipoanzishwa.
Akizungumza leo Jumapili, Januari 18, 2026, akiwa mgeni rasmi katika mjadala wa kidijitali kuhusu historia ya kuanzishwa kwa mabaraza ndani ya Chadema na mchango wake, Lyimo amesema mjadala huo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya kuanzishwa kwa chama hicho, ambayo kilele chake kinatarajiwa kufanyika Januari 21, 2026.
Amesema hali hiyo imeendelea kudhoofisha ushiriki wa wanawake katika uongozi wa juu wa chama, licha ya mchango mkubwa walioutoa katika kukijenga na kukiendesha kwa miaka mingi.
“Nimesema na nitarudia kusema, nawaomba viongozi wangu wanaume wanisikie. Tunaonekana kama wanawake wa ajabu, kwamba wanawake wa Chadema wana uwezo mkubwa lakini hawaonekani katika ngazi za juu za chama,” amesema Lyimo.
Kwa mujibu wake, ingawa katiba ya chama inaruhusu nafasi za kugombea, bado nafasi za uteuzi kama Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu hazitolewi kwa wanawake, hali ambayo amehoji mantiki yake.
“Ni kweli kuna nafasi za kugombea, lakini kwenye nafasi za uteuzi kama Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu, inakuwaje wanawake hawapewi nafasi hizo?” amehoji.
Akieleza kuhusu jitihada zake binafsi, Lyimo amesema katika uchaguzi wa ndani ya Chadema uliofanyika Januari 21, 2025, alizungumza na Mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu pamoja na Mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe akitafuta suluhisho ya changamoto hiyo wakati wakisubiri matokeo ya uchaguzi.
“Niliwaambia waheshimiwa tumekuwa tukisemwa vibaya kwamba chama chetu kina mfumo dume. Niliwaomba yeyote kati yao atakayeshinda kwenye zile nafasi za uteuzi, angalau awepo mwanamke hata mmoja,” amesema.
Hata hivyo, anasema licha ya kukubaliana naye, utekelezaji wa makubaliano hayo haukuwa kama ilivyotarajiwa, jambo ambalo anasema halikumvunja moyo.
“Nilienda tena kuzungumza na Lissu kwa kuwa ndiye aliyeshinda, nikamuuliza tulikubaliana imekuwaje? Alichonijibu nisingependa kukisema hapa kwa sababu watu wanatusikiliza, ingawa alikuwa mtu chanya zaidi,” amesema.
Kwa mujibu wa Lyimo, Lissu alimweleza kuwa alikuwa tayari kuteua mwanamke, lakini mazingira yaliyokuwapo wakati huo hayakumruhusu kutekeleza azma hiyo.
“Bado ninarudia kilio changu kipo palepale. Wanawake wa Chadema ni majasiri, wapewe fursa katika nafasi zile tano za juu. Kama tumekosa mwenyekiti au makamu mwenyekiti, basi hata katibu mkuu au naibu katibu mkuu bara au Zanzibar,” amesisitiza mwenyekiti huyo.
Amesema nafasi hizo ni muhimu kwa wanawake kwa kuwa zinatoa mfano wa kuigwa kwa wanachama wengine huku akibainisha kwamba, kukosekana kwa mwanamke katika uongozi wa juu kumekuwa kukiwakatisha tamaa.
Katika hatua nyingine, Lyimo amewapongeza wanawake wa Chadema waliobaki imara ndani ya chama mpaka sasa, akisema walipitia dhoruba kali lakini wameendelea kusimama imara.
“Chama kimekuwa kikizungumzwa na wananchi na kinategemewa muda wote. Kama tunaweza kuandaa ilani, itakuwaje tushindwe kushika nyadhifa za juu wakati kuna wasomi wengi wanawake?” amehoji Lyimo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bwawacha), Sharifa Suleiman amesema baraza hilo linasimama imara sambamba na Watanzania wote katika kuongoza mapambano ya kupigania na kutetea haki zao za msingi.