Namba za Stumai Abdallah Ligi Kuu ya Wanawake

MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu uliopita, Stumai Abdallah hajafikia kiwango alichokionyesha msimu uliopita baada ya kuanza msimu huu kwa kufunga bao moja na asisti nne.

Hadi sasa, Stumai amefunga bao moja pekee katika mechi nane alizocheza, tofauti na msimu uliopita na hadi raundi hii tayari alikuwa amefikisha mabao 11, takwimu zilizomfanya kuwa tishio kwa safu za ulinzi za wapinzani.

Mabadiliko ya kiwango chake yanaonekana kuchangiwa na mabadiliko ya majukumu katika timu na Kocha Kessy Abdallah ameonekana kumbadilishia nafasi ya uchezaji.

Tofauti na ilivyokuwa awali alikuwa akicheza kama mshambuliaji wa mwisho, msimu huu Stumai anacheza zaidi kama kiungo mshambuliaji.

Kwa sasa kinda Jamila Rajabu amekuwa akitumika kama mshambuliaji hali inayomlazimu Stumai kushuka nyuma zaidi kusaidia kiungo na kusambaza pasi.

Hata hivyo, mchango wa Stumai bado unaonekana katika uchezaji wa jumla wa timu, akihusika katika kujenga mashambulizi, kutoa pasi za mwisho na kuvunja safu za ulinzi za wapinzani.