Namungo yamwinda mido Chama la Wana

WAKATI zikibakia takribani wiki mbili kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Januari 30, 2026, mabosi wa Namungo wamefungua mazungumzo rasmi ya kuipata saini ya kiungo mshambuliaji wa kikosi cha Stand United ‘Chama la Wana’, Shaban Zubery Ada.

Nyota huyo aliyeifungia Stand United bao moja katika Ligi ya Championship msimu huu, ni miongoni mwa wachezaji wanaohitajika na timu hiyo inayonolewa na Kocha Juma Mgunda kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la kiungo ushambuliaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman amesema kuna baadhi ya wachezaji wako katika mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kupata saini zao, hivyo muda wowote kuanzia sasa wataweka wazi kwa wale waliowasajili dirisha hili lililofunguliwa Januari 1, 2026.

“Kuna baadhi ya taratibu ambazo tunaendelea kuzikamilisha na hivi karibuni tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuweka wazi nyota wote tuliowasajili, tunaboresha baadhi tu ya maeneo kadhaa kutokana na ripoti ya benchi la ufundi,” amesema Ally.

Kiungo huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali za Lipuli, Mbeya City na Geita Gold, ni miongoni mwa viungo wanaosifika kwa uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao, jambo linalosababisha Namungo kuisaka saini yake katika dirisha hili.

Mwanaspoti linatambua, mbali na Shaban, Namungo imeinasa saini ya kipa, Ahmed Feruz aliyekuwa anaichezea pia Stand United kwa ajili ya kuongeza nguvu katika eneo hilo, huku nyota huyo akiwahi kuchezea pia timu za Simba na Kagera Sugar.