Dar es Salaam. Benki ya NMB imetangazwa kuwa mwajiri bora Tanzania kwa mwaka wa tatu mfululizo kupitia tuzo za kimataifa za waajiri 2026 zinazotolewa na taasisi ya Top Employers Institute, zilizotangazwa wiki hii.
Cheti hicho cha mwajiri bora, kinachotolewa na taasisi ya kimataifa iliyobobea katika ubora wa rasilimali watu, kinaifanya NMB kuwa miongoni mwa takribani mashirika 2,500 duniani yaliyotunukiwa heshima hiyo mwaka huu.
Top Employers Institute ni taasisi ya kimataifa inayotambua ubora wa usimamizi wa rasilimali watu, ikifanya tafiti na ukaguzi huru wa sera na mifumo ya kampuni ili kuhakikisha zinazingatia viwango vya kimataifa.
Kwa miaka mitatu mfululizo, NMB imetunukiwa cheti hicho cha mwajiri bora, jambo linaloonesha si tu mafanikio yake ya sasa, bali pia dhamira yake thabiti ya kujenga na kuendeleza mazingira bora ya kazi yanayozingatia ubora, ushirikishwaji na ustawi wa wafanyakazi wote.
Cheti cha Mwajiri Bora, ambacho kimetolewa kwa zaidi ya miaka 33, hutambua taasisi zinazowajali wafanyakazi wao kwa kusimamia vizuri rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kazi.
Mchakato wa tathmini ulijumuisha maeneo sita makuu ya rasilimali watu katika vipengele 20 vya sera na mbinu za usimamizi wa wafanyakazi wa benki.
Maeneo hayo ni pamoja na mkakati wa watu, uajiri wa vipaji, maendeleo ya wafanyakazi, usimamizi wa vipaji, ustawi wa wafanyakazi, usawa na ujumuishaji, pamoja na mazingira bora ya kazi.
Akizungumza kuhusu mafanikio haya makubwa, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema wanajivunia kupata cheti hicho tena, akisema kuwa mafanikio hayo yanaonesha dhamira yao ya kuendeleza mazingira bora ya kazi.
“Mafanikio haya yanaonesha dhamira yetu thabiti ya kuwa na kuendeleza mazingira ya kazi yanayokuza ubora, huku mifumo yetu ya rasilimali watu ikiweka viwango vya sekta. Tuzo hii ni matokeo ya jitihada za pamoja.
“Tusingefanikisha hili bila wafanyakazi wetu bora, ambao si tu wameweka viwango vipya ndani ya NMB, bali pia wana utamaduni imara wa kazi unaoonesha juhudi zao za kufanikisha ubora. NMB itaendelea kujitolea katika ubora, kukuza usawa na ujumuishaji, na kuwawezesha wafanyakazi wake kujenga mustakabali bora,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Emmanuel Akonaay, amesema: “Kupata heshima hii kwa mwaka wa tatu mfululizo kunathibitisha dhamira ya NMB ya kudumisha viwango vya juu katika sekta.
“Pia inaonesha jinsi tunavyowathamini wafanyakazi wetu, tukiwekeza si tu katika teknolojia na ubunifu, bali pia katika maendeleo yao ya kitaaluma na ustawi wa zaidi ya wafanyakazi 5,000 wa benki.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Top Employers Institute, Adrian Seligman, amesema: “Kupata cheti cha Taifa cha Mwajiri Bora kwa mwaka 2026 kunaonesha dhamira ya Benki ya NMB ya kujenga mazingira bora ya kazi yanayosaidia mafanikio endelevu ya biashara.
“Tunajivunia kuitambua Benki ya NMB kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha mazingira ya kazi Tanzania.”