Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewataka wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kutumia ipasavyo muda wao wa masomo kwa kujifunza uchambuzi wa takwimu (Data Analysis), usalama wa taarifa pamoja na mbinu za ununuzi wa umma, ili kujiandaa na fursa zilizopo katika soko la ajira na biashara za Serikali.
Wito huo umetolewa leo Jumapili, Januari 18, 2026 na Mkurugenzi wa PPRA, Dennis Simba, wakati wa kuwapatatia mafunzo ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Biashara (CBE), yaliyolenga kuwaelimisha kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta ya manunuzi ya umma.
Simba amewahimiza vijana hao kuanzisha vikundi vya kiuchumi vyenye wanachama kati ya watano hadi 20 kulingana na maeneo wanayoyamudu, kisha kuvisajili ili viweze kuingizwa katika mfumo maalumu wa Serikali unaowawezesha kushiriki ushindani wa zabuni na huduma mbalimbali.
Amesema PPRA imeanza kutoa mafunzo hayo katika vyuo viwili kwa awamu ya kwanza, huku mipango ikiwa ni kufika katika vyuo vikuu vyote nchini, akibainisha kuwa tayari mamlaka hiyo imeanza kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) na Chuo cha Biashara(CBE) wakimsikiliza Mkurugenzi wa PPRA Dennis Simba jijini Dodoma.
Akizungumzia mabadiliko ya teknolojia, Simba amesema kizazi cha sasa ni cha kidijitali, hivyo ni wajibu wa vijana hao kuchangamkia fursa zinazotokana na matumizi ya Tehama katika manunuzi ya umma na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wao wanafunzi wamesema elimu waliyoipata kuhusu mbinu za manunuzi ya umma itawasaidia kujiandaa vyema na ushindani wa soko la ajira.
“Mafunzo haya yametupa uelewa mpana kuhusu namna vijana tunavyoweza kuungana na kuanzisha vikundi vya kitaaluma vitakavyowawezesha kushiriki katika zabuni na huduma za Serikali.” amesema Selina Misalaba
Ameongeza kuwa “Tumejifunza kutohitaji kusubiri kuajiriwa pekee, bali tunaweza kuunda vikundi vyetu, kuvisajili na kuingia moja kwa moja kwenye mifumo ya manunuzi ya umma.”