KILICHOTOKEA msimu wa 2012-2013 katika Ligi Kuu Bara, kinabaki kuwa kumbukumbu nzuri kwa Mtibwa Sugar inapokwenda kucheza dhidi ya Simba leo Jumapili kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar kwani kipindi hicho iliibuka na ushindi nyumbani na ugenini dhidi ya wapinzani wao hao.
Kipindi hicho, Mtibwa ilianza kuifunga Simba mabao 2-0 nyumbani, Novemba 4, 2012, kisha Februari 24, 2013 ikashinda 1-0 ugenini.
Baada ya hapo, Mtibwa haijawahi kupata ushindi kwenye ligi dhidi ya Simba zikikutana mara 22. Katika mechi hizo, Simba imeshinda 15 na sare saba, haijapoteza.
Leo timu hizo zinakutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam huku yakitarajiwa kupatikana mabao ya kutosha kutokana na rekodi zao za hivi karibuni, lakini pia kile walichozungumza makocha wa timu zote mbili katika suala zima la kusaka ushindi.
Simba ambayo ni timu mwenyeji, inaingia uwanjani ikiwa na benchi jipya la ufundi likiongozwa na kocha mkuu, Steve Barker ambaye hii ni mechi yake ya kwanza Ligi Kuu Bara tangu atambulishwe Desemba 19, 2025 akichukua mikoba ya Dimitar Pantev.
Hata hivyo, tayari Barker ameshaiongoza Simba katika mechi tatu za Kombe la Mapinduzi 2026, timu hiyo ikiishia hatua ya nusu fainali ikifungwa na Azam bao 1-0. Kabla ya hapo ilishinda mbili dhidi ya Muembe Makumbi City (1-0) na Fufuni (2-1).
Katika mechi kumi za mwisho Simba kucheza na Mtibwa kwenye ligi, moja pekee imemalizika bila bao, huku zilizobaki nyavu zimetikiswa kuanzia mara mbili, Simba ikishinda nane, sare mbili. Mtibwa haijaonja ladha ya ushindi.
Akizungumzia mechi hiyo, Barker alisema: “Tumepata muda mzuri wa kujiandaa baada ya wachezaji waliokuwa timu ya taifa kurejea, tumekuwa na kikosi imara wakati wa maandalizi kuelekea mechi ya kesho (leo), tunapaswa kuanza vizuri mechi yetu ya kwanza ya ligi mwaka huu.
“Tunakwenda kucheza dhidi ya timu ngumu kufungika, lakini tumeifanyia uchambuzi wa kina na tutaiuliza maswali mengi hasa eneo la ushambuliaji japo wana safu nzuri ya ulinzi na kocha mzuri.
“Mechi haitakuwa rahisi, tunachotakiwa kufanya ni kucheza kwa kujiamini na kucheza nyumbani kwetu ni faida. Tutafanya kila liwezekanalo kushinda.
“Sowah na Kante wana adhabu, wengine wawili wanarejea kutokea kwenye majeraha, Morice ni kati yao ameanza mazoezi na yupo karibu kuingia katika kikosi kwa ajili ya mechi, tutamfanyia tathmini katika mazoezi ya mwisho kabla ya kufanya uamuzi wa kucheza au la.”
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Yusuf Chipo, alisema: “Tumejiandaa vizuri, tunafahamu tunacheza na timu kubwa Simba, na sisi tuna jambo letu hapo kesho (leo). Wana benchi jipya na tumeona mechi zao za Kombe la Mapinduzi, naamini itakuwa mechi tofauti kwani wamebadilika kimbinu kutokana na kuwa na kocha mpya.