UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Mambo haya 4 yakifanyika, tutaponya majeraha ya Oktoba 29

Hakuna ubishi kuwa taifa limegawanyika, watu wana maumivu makubwa mioyoni mwao kutokana na yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata na jitihada za kulileta taifa pamoja zinaendelea, lakini kuna mambo tunakwepa kuyafanya.

Kuna vidonge vinne tu ambavyo taifa likipewa vitatuliza maumivu, kusameheana na kuanza upya navyo ni watawala kukiri makosa, kuomba radhi, kulipa fidia waathirika na kuwawajibisha watakaoonekana walitenda ndivyo sivyo.

Ni lazima kuanzia sasa, viongozi wetu wazungumze lugha ya kukiri kuna mahali tuliteleza na si kutizama tulipoangukia, na kauli za kulaumu tu hazitatusaidia kurejesha umoja, mshikamano na upendo tuliokuwa nao, tutazidi kuligawa.

Matukio ya siku ya uchaguzi Oktoba 29,2025 na ya siku zilizofuata yameliacha taifa letu katika maumivu makubwa lakini bahati mbaya sana, wapo viongozi wetu bado wako katika hali ya kutokubali makosa (state of denial) na kuzidisha maumivu.

Hata katika kutafuta maridhiano ya wanandoa, wazee wanaosuluhisha mgogoro huo ni lazima watasikiliza upande wa mume na mke na kuweka rula katikati na mkosaji anatubu kosa alilofanya, wanasameheana, maisha yanaendelea.

Ni kweli kuwa siku hiyo wapo vijana wa kizazi cha sasa (Gen Z) waliandamana bila kufuata utaratibu wa sheria na kuvilazimisha vyombo vya usalama kutumia nguvu kuzima kile walichokiita ni maasi ya kutaka kuipindua Serikali kwa maandamano.

Siku zote msafara wa mamba huwa kenge hawakosekani, kwani miongoni mwa waandamanaji hao, kulikuwepo waliotumia fursa hiyo kuharibu na kupora mali na katika makabiliano hayo, wapo baadhi yao waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Kama matumizi ya nguvu yalikuwa ni halali ama la, huo ni mjadala mwingine.

Taarifa ya awali ya Waziri mkuu, Dk Mwigulu Nchemba inaonyesha ofisi za Serikali 756 zilichomwa sambamba na vituo vya mabasi ya mwendo kasi (BRT) 27), mabasi 6, nyumba binafsi 273, vituo vya Polisi 159 na vituo vya kuuza mafuta 672.

Uharibifu mwingine ni magari ya watu binafsi 1,642, pikipiki binafsi 2,268 na magari ya Serikali 976. Hakika huu ulikuwa ni uharibifu mkubwa na unaumiza.

Hilo ni kundi la kwanza, lakini kundi la pili ni la wananchi wasio na hatia kabisa, hawakuwepo kwenye maandamano na wala wengine walikuwa hata hawajui kuna maandamano, ambao waliuawa mitaani na wengine risasi ziliwapata majumbani.

Serikali imejitahidi sana kuonyesha ukubwa wa mali zilizoharibiwa lakini haioni umuhimu wa kutaja idadi ya watanzania waliofariki kwani hiyo ingesaidia pia Serikali, watanzania na jumuiya za kimataifa, kupima ukubwa wa tatizo.

Msema kweli ni mpenzi wa Mungu na nasema hili kwa nia njema kabisa kwamba moja kati ya mambo ambayo yanaleta hasira ni kuficha idadi ya waliokufa na miili yao iko wapo ili ndugu waweze kuwazika wapendwa wao kwa heshima.

Kanuni kubwa kabisa katika kutafuta maridhiano ni kukiri na kukubali makosa na wala kufanya hivi si udhaifu, kwani kunafanya yule uliyemkosea aone kweli unajutia (remorse) kile ulichomfanyia ili sasa arejeshe moyo na kusamehe.

Lakini tukiendelea kuwa katika “state of denial” (kuukataa ukweli) wakati watanzania wa leo wa kizazi cha digitali wanafahamu kila kilichotendeka, ni kutatua matatizo yetu kwa kujifanya kama hayapo kama Nyerere alivyosema.

Ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukiri kuna tatizo ndio maana akaunda Tume kuchunguza vurugu hizo za Oktoba 29, lakini kuna kauli zinaendelea kutolewa ambazo zinaondoa kabisa maana na umuhimu wa Tume.

Lakini natamani Rais aunde Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC) kama iliyoundwa Afrika Kusini hasa tukimnukuu Askofu Desmond Tutu akisema “Without truth, there can be no reconciliation”, akimaanisha bila ukweli hakuna maridhiano.

Nafahamu Rais anasubiri ripoti ya Tume aliyoiunda kuchunguza vurugu za Oktoba 29 ikiongozwa na Jaji mkuu mstaafu Othman Chande, ni muhimu tume hiyo ikatoa sura ya maridhiano ya kweli na isibue maswali na hisia hasi kama tume hiyo.

Ninasema hivyo kwa sababu mijadala mitandaoni na kwa wananchi wa kawaida ni ya moto huko mitandaoni kuhusu wajumbe wa Tume hiyo na uungwaji mkono.

TRC ya Afrika Kusini iliundwa mwaka 1995 kufuatia kumalizika kwa ubaguzi wa rangi na ilianzishwa chini ya sheria ya ujenzi wa umoja wa Kitaifa na Maridhiano.

Tume hii ililenga kutoa jukwaa (platform) kwa waathiriwa kueleza madhila waliyoyapitia wakati wa zama za ubaguzi wa rangi uliodumu kati ya mwaka 1960 na mwaka 1994 na wahalifu kukiri makosa yao na kuomba msamaha.

Kulingana na takwimu zilizopo, Tume hii ilipokea maelezo zaidi ya 21,000 kutoka kwa waathirika na kusikiliza ushuhuda wa watu 2,000 kwa njia ya wazi na Tume ilitoa msamaha kwa watu 849 walioshiriki au kuhamasisha uhalifu kipindi hicho.

Ndio maana nimetangulia kusema pale mwanzo, kwamba kuna dawa 4 tukilipa taifa letu leo, ndio itakuwa tiba ya majeraha waliyonayo watanzania na chuki za visasi walizonazo kutokana na mauaji ya ndugu zao na kutopata miili yao.

Kwa hiyo tukiunda tume ya ukweli, narudia tena ya ukweli ya maridhiano, itakuwa fursa nzuri kwa Polisi na wengine wa vyombo vya usalama, kufika mbele ya Tume kujenga hoja ya kuhalalisha (justification) ya kile walichokifanya Oktoba 29.

Tunasema hivyo kwa sababu sio maofisa wote wa vyombo vya Usalama walitumia nguvu kupita kiasi, hapana, tunao maofisa wengi tu ambao hawakushiriki katika udhibiti ule wala kusababisha mauaji hivyo tusiwachanganye katika kapu moja.

Wale watakaoonekana walitenda kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi na wakakiri makosa yao na kuomba msamaha, basi wasamehewe maisha yaendelee, lakini wale watakoonekana walikiuka kwa makusudi, basi wawajibishwe.

Sasa wakishakiri makosa, wakaomba radhi na wale watakaoonekana hawa hapana hawakutumwa ku “shoot and kill” na wakasamehewa, basi Serikali iwajibike kutoa fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na vile vile kwa majeruhi.

Lakini tutumie maridhiano hayo hayo, kuridhiana kuhusu matendo mabaya ya kisiasa ambayo tumefanyiana tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992 hadi sasa ikiwamo kukandamiza vyama vya upinzani na wagombea wao.

Tutumie maridhiano hayo kuridhiana juu ya utendaji wa Jeshi letu la Polisi na vyombo vingine vya usalama ambavyo vinanyooshewa kidole kwa matukio ya utekaji wa watu, kupotea kwa watu, mateso na mauaji ya raia wasio na hatia.

Tuambiwe ndugu zetu waliotekwa au kupotezwa wako wapi, kama walitumbukizwa katika mto wenye mamba tuambiwe au kama wako kwenye jumba wamefungiwa huko, basi waachiliwe mara moja maisha yaendelee.

Lakini twende mbali zaidi tutumie maridhiano hayo kurudisha utawala wa sheria na kurejesha mchakato wa kuandika Katiba mpya, ambavyo vitatusaidia kuwa na taasisi imara (strong institution) hasa hasa Bunge Huru na Mahakama Huru.

Tume Huru ya Uchaguzi (sio kwa jina bali sifa) utatuletea uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika na utatuondolea migogoro ya kisiasa kama tuliyoishuhudia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020 na 2025.

Tunayafanya haya tukitambua kuwa hakuna mtanzania anayependa kuishi katika taifa lililovimba ambalo watu wananuiana visasi na hili wala halihitaji “rocket science”, kwani ukiingia kwenye mitandao ya kijamii utapata ushahidi huo.

Leo hii kiongozi wa Serikali, CCM na watendaji na maofisa wa vyombo vya usalama wakipata madhila watu wanafanya sherehe mitandaoni na baadhi ya viongozi wanafunga eneo lile la watu kutoa maoni (comments section) kwenye akaunti zao.

Hii si dalili njema hata kidogo na hata aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alizungumzia hili na akatolea mfano wa Polisi akipata ajali sasa hivi badala ya wananchi kumsaidia, wao wanashangilia.

Ni lazima tufike mahali tutambue kuwa ni kutenda haki pekee ndio kutazaa amani tunayoitamani na wala tusijivune kuwa tuna amani bali tutambue tuna utulivu na ni lazima tutambue Tanzania ni yetu sote hakuna mtu mwenye hati miliki nayo.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900