Ushindi wa Museveni wawaibua wasomi, wamulika demokrasia Afrika

Dar es Salaam. Ushindi wa kiongozi wa Uganda wa muda mrefu, Yoweri Museveni (81), umewaibua wachambuzi wa siasa wanaoeleza kuwa ushindi huo ulitarajiwa na kwamba unaakisi demokrasia na siasa za Afrika.

Jana, Januari 18, 2026, Museveni ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Januari 15, 2026, na hivyo kuongeza muda wake wa uongozi kuvuka zaidi ya miongo minne madarakani.

Museveni, kiongozi wa zamani wa waasi aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya vita vya msituni vya miaka mitano, alitangazwa mshindi Jumamosi iliyopita kufuatia uchaguzi uliokuwa na mvutano mkubwa na uliofanyika huku intaneti ikiwa imezimwa kote nchini humo.

Rais Museveni akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Karo huko Rwakitura Januari 15, 2026. PICHA/SCREEN-GRAB/UBC



Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Simon Byabakama, alisema Museveni alipata kura 7,944,772, sawa na asilimia 71.65 ya kura zote halali zilizopigwa.

Kwa mujibu wa Jaji Byabakama, jumla ya Waganda 11,366,201 walipiga kura, idadi inayowakilisha asilimia 52.5 ya wapigakura waliojiandikisha.

Mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine wa chama cha National Unity Platform (NUP), alipata kura 2,741,238, sawa na asilimia 24.72 ya kura zote zilizopigwa.

Bobi Wine, ambaye alisema alilazimika kuikimbia nyumba yake kufuatia uvamizi wa polisi na jeshi usiku wa kuamkia Ijumaa, amepinga matokeo hayo akidai si ya kweli. Katika taarifa aliyotoa Jumamosi alasiri kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Bobi Wine alisema alitoroka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya Wakiso, baada ya kupata taarifa kuwa maofisa wa utawala walikuwa wakimsaka.

Matokeo hayo ya uchaguzi yamewaibua wasomi wanaochambua kwa kina miaka mitano ijayo ya Rais Museveni, mrithi wake wa baadaye na nafasi ya demokrasia katika nchi hiyo yenye watu zaidi ya milioni 48.7.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Dk Abdallah Mkumbukwa, amesema ushindi wa Rais Museveni katika uchaguzi ulitarajiwa licha ya kampeni zake kutokuwa na hamasa kubwa.

Dk Mkumbukwa amesema tangu awali Museveni alitarajiwa kushinda ikilinganishwa na mpinzani wake, Bobi Wine, ambaye kampeni zake zilitawaliwa na figisufigisu, ndicho kilichojitokeza.

“Matarajio yalikuwa wazi, Museveni angeshinda na ndivyo ilivyotokea. Mpinzani wake alikuwa na nguvu zaidi katika maeneo ya mijini, ambako ndiko alikojijengea ushawishi mkubwa na kuungwa mkono na vijana wengi,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mkumbukwa, chama kinachoongozwa na Museveni, cha National Resistance Movement (NRM), kimejiimarisha katika maeneo mengi ya nchi, hususan vijijini, ambako pia kuna idadi kubwa ya vijana.

Rais Museveni akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Karo huko Rwakitura Januari 15, 2026. PICHA/SCREEN-GRAB/UBC



Amesema katika nchi nyingi za Afrika, asilimia kubwa ya wananchi wanaishi vijijini, ndiyo sababu ya vyama vilivyokita mizizi huko kushinda chaguzi.

“Wananchi wa vijijini hutegemea kilimo kama chanzo kikuu cha maisha yao, hivyo wanahitaji usalama na amani ili watekeleze shughuli zao. Ndiyo maana bado wana imani na chama cha Museveni, licha ya kukaa madarakani kwa muda mrefu,” amesema.

Ushirikiano wa kisiasa na maendeleo

Mwanadiplomasia mwandamizi, Balozi Benson Bana, amesema Museveni alikuwa kiongozi aliyetarajiwa kutokana na misingi aliyojijengea tangu enzi za watawala waliomtangulia pamoja na mapambano ya muda mrefu ya kisiasa nchini humo.

Balozi Bana amesema Rais huyo alipoingia madarakani aliipa Uganda mwelekeo mpya kwa kushughulikia masuala ya ukabila na udini, jambo lililosaidia kuimarisha umoja wa kitaifa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

“Museveni alichukua madaraka, akaiongoza Uganda kwa kuweka sawa masuala ya ukabila na udini, akajenga uchumi unaoendelea kupaa, na sasa nchi imegundua rasilimali ya mafuta,” amesema Balozi Bana.

Ameeleza Museveni ni kiongozi thabiti asiyeathiriwa na shinikizo au kauli za mataifa makubwa, huku akisema mtu yeyote anayetembelea Uganda anaweza kushuhudia mabadiliko makubwa ya maendeleo.

“Maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanaonekana wazi. Ndiyo maana Museveni anaendelea kupata kura nyingi, licha ya wimbi la madai ya mageuzi ya vijana. Wananchi wa Uganda wanajua wanamtaka nani,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Denis Konga, amesema demokrasia ya Afrika ni tofauti na ile ya Magharibi, kwa kuwa haijajikita kikamilifu katika kuangazia maisha, maslahi na mitazamo ya wananchi.

Afisa wa polisi na wanajeshi wanaonekana katika kituo cha kupigia kura mjini Kampala Januari 15, 2026, kabla ya uchaguzi wa kitaifa. PICHA/ABUBAKER LUBOWA



Konga amesema mara nyingi kiongozi aliyepo madarakani huwa na nguvu na uhakika mkubwa wa kushinda uchaguzi, kwa sababu ndiye mwenye mamlaka ya kuteua wajumbe wa Tume ya Uchaguzi na pia kutoa rasilimali zitakazowezesha tume hizo kufanya kazi.

“Katika demokrasia ya Afrika, anayekuwa madarakani ndiye mwenye nguvu. Yeye ndiye anateua tume na ana uwezo wa kuipatia rasilimali ili iweze kufanya kazi,” amesema Konga.

Amesema vyombo vya habari katika baadhi ya nchi za Afrika hukosa uhuru wa kuandika au kuripoti kwa haki, hasa pale vinapojaribu kuonesha mafanikio au upungufu kwa mtazamo tofauti na ule wa serikali iliyopo madarakani.

Kwa upande mwingine, Konga amesema vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mengi ya Afrika vimekuwa vikihusishwa na siasa, mara nyingi vikionekana kuunga mkono chama kinachotawala.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa sehemu ya siasa za walioko kwenye madaraka. Lengo lao kubwa huwa ni kulinda nafasi zao badala ya maslahi ya taifa,” amesema.

Amesema hali hiyo inachangiwa na hofu miongoni mwa watumishi wa umma, ambao huogopa hatima yao endapo uongozi utabadilika.

“Kuna msemo usemao ‘amlipaye mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo’. Serikali iliyopo madarakani ndiyo yenye uwezo wa kulipa. Pia, kuna ule msemo wa ‘zimwi likujualo halikuli, likakwisha’, hivyo watumishi hujiuliza kama wataendelea kufaidika au kuondolewa endapo kiongozi mpya ataingia,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Konga amesema watumishi wengi huamua kuendelea kumuunga mkono kiongozi aliyepo madarakani ili kulinda nafasi zao.

Akizungumzia suala la urithi wa madaraka nchini Uganda, Konga amesema haoni uwezekano wa Museveni kuachia madaraka baada ya muda wa miaka mitano.

“Kwa mtazamo wangu, Museveni hawezi kuondoka madarakani labda Mungu afanye yake. Sioni kama anaweza kuachia ngazi,” amesema.

Akizungumzia hatima ya Uganda baada ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Museveni, Dk Mkumbukwa amesema ni vigumu kubashiri itakuwaje kwa sababu kiongozi yuleyule aliyekuwepo ndiyo anaendelea.

“Viongozi waliokaa madarakani muda mrefu mara nyingi hawana mambo mapya, lakini kwa sababu Uganda imegundua mafuta wakati wa utawala wa Museveni, atatumia rasilimali hiyo kubadilisha maisha ya watu wake,” amesema.

Kwa upande wake, Balozi mstaafu, Dk Bana, amesema mustakabali wa Uganda utaamuliwa na wananchi wenyewe, na kama wanamhitaji Museveni, wataendelea kumchagua tena na tena, kwani hawaoni mwingine.

“Shida ya Museveni siyo kukaa muda mrefu, bali ni nani anayefaa zaidi yake? Nafikiri hicho ndiyo kitu kikubwa cha kukiangalia katika siku zijazo, kwa sababu lazima awepo mtu atakayebeba maisha na ndoto za Waganda,” amesema.