Dar es Salaam. Ugumu umeendelea kuyatawala mazungumzo kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Chama cha ACT- Wazalendo kuhusu mwafaka wa chama hicho kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Hiyo ni baada ya ACT – Wazalendo kuweka wazi kuwa, haijaafikiana na Serikali kuingia SUK, kwa kile kilichoelezwa na viongozi wake kuwa, bado Serikali ya Zanzibar haijajibu matakwa yao.
ACT – Wazalendo inakuja na msimamo huo, wakati ambao jana, Jumapili Januari 18, 2026 ndio iliyotarajiwa kuwa siku ambayo kingetoa kauli ya kuingia SUK, baada ya mvutano wa takriban mwezi mmoja na Serikali ya Zanzibar.
Hali imeendelea kuwa ngumu, ingawa zimesalia siku 22 kati ya zile 90 ambazo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, ACT Wazalendo iliyopata zaidi ya asilimia 10 ya kura za Rais wa Zanzibar inapaswa kuingia SUK.
Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita akizungumza kwenye kikao cha Kamati Kuu kinachoendelea muda huu Makao Makuu ya ACT Wazalendo Magomeni Dar es Salaam.
Hata hivyo, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi, alipoteua Baraza la Mawaziri, aliacha nafasi nne zitakazozibwa na wajumbe kutoka chama hicho kikuu cha upinzani.
Mwananchi imezungumza na wajumbe kadhaa wa kamati kuu waliokuwa sehemu ya kikao hicho, wamesema hakuna mwafaka uliofikiwa, hivyo bado hakijaeleweka kuhusu chama hicho kuingia SUK.
Kwa mujibu wa viongozi hao walioomba hifadhi ya majina yao, kutofikiwa kwa mwafaka huo, kumetokana na Serikali kutotimiza watakwa ya chama hicho, ambayo hata hivyo hawajayaweka wazi.
“Bado hawajajibu matakwa yetu. ACT- Wazalendo bado tunavutana na Serikali kuhusu kuingia GNU (SUK),” amesema kiongozi huyo aliyekuwa katika kikao hicho cha kamati kuu.
Hadi saa 12:15 jioni jana, bado kikao hicho kilikuwa kinaendelea, lakini msimamo wa chama hicho hadi muda huo, ni kwamba hawataingia SUK hadi matakwa yao yatakapotimizwa.
Mvutano wa ACT-Wazalendo na Serikali ya Zanzibar kuingia katika SUK, ulianza mapema Novemba mwaka jana, baada ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Balozi Zena Ahmed Said kukiandikia barua chama hicho ili kipeleke jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Hata hivyo, Novemba 13, 2025, Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman aliwaambia wanachama akiwa ziarani Pemba visiwani humo kuwa, hawakupeleka jina wakati huo, kwa madai ya kutoridhishwa na mazingira ya kisiasa.
Baada ya mvutano huo, chama hicho kilipanga kikao cha kamati kuu kilichofanyika Januari 17 na 18 mwaka huu, kujadili pamoja na mambo mengine, uamuzi wa mwisho kuhusu ama kuingia SUK au vinginevyo.
Lakini, kikao hicho si cha kwanza, kamati ya uongozi ya chama hicho, ilishaketi Novemba 23, mwaka jana visiwani Zanzibar kutathmini kuhusu uchaguzi na iligusia suala la SUK, ingawa sio kwa mapana yake.
Mapema mwezi huu, Mwananchi ilizungumza na mmoja kati ya viongozi wa chama hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa chama, alisema ACT-Wazalendo imeweka masharti kadhaa ili kuingia SUK na baadhi inadaiwa yameshaanza kutekelezwa, ingawa hajayaweka wazi.
Kwa sababu hiyo, kiongozi huyo alisema inakifanya chama hicho kitangulize mguu mmoja ndani ya SUK, huku jitihada nyingine zikiendelea kuhakikisha mwafaka baina ya pande zote unafikiwa.
Hata hivyo, alieleza kumekuwa na juhudi za kila namna zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar kuishawishi ACT-Wazalendo iingia SUK ikiwamo kuwatumia wazee maarufu wa Bara na Zanzibar na watu wengine maarufu.
Pia, alisema wapo viongozi wasiotaka kabisa chama hicho kiingie SUK kwa sababu wanadai walidhulumiwa uchaguzi, hivyo ziendelee juhudi za kudai haki.
Alisema chama hicho kimefungua kesi mbalimbali za uchaguzi kushinikiza kupatikana kwa haki zake, wakati huo huo kimeshatanguliza mguu kuingia SUK, bila kuathiri mapambano ya kudai haki.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo mapema mwezi huu, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita alisema msimamo wao ni kwamba, kabla ya kuingia au kutoingia, wanaangalia iwapo kwa mazingira yaliyopo sasa malengo ya kuanzishwa SUK yatafikiwa.
Alieleza SUK ilianzishwa kuepusha mitafaruku na migogoro ya kisiasa na kijamii, uhasama wa kiraia na kinachofanywa na ACT- Wazalendo ni kutathmini iwapo hatua yao ya kuingia mwaka 2020 imeleta matokeo chanya.
Mwenyekiti Mstaafu wa Babu Duni akizungumza kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika leo Makao Makuu ya Chama Magomeni Dar es salaam.
Kwa tathmini yao, alisema wanaona pamoja na chama hicho kuingia SUK 2020, hakuna matokeo chanya yaliyopatikana, hivyo wanatafakari kuona je, wanapaswa kuingia kwa namna ile ile au kwa namna ipi itakayoleta tija kwa umma.
“Tunaona kuingia kwa namna tulivyoingia hatuoni malengo ya kuanzishwa kwa SUK yakitimia. Ikiwa kuingia kwa namna ya zamani itakuwa muarobaini tutaingia, lakini ikiwa kuingia ni kwa sababu ya kupeana vyeo haitakuwa na maana.
“Tuko tayari kujadiliana kwenye eneo hilo na zipo hatua zinazochukuliwa ingawa ni za ndani kwa sasa, tunatazama na kuona kama itafika hatua ya kutoa taarifa kwa umma,” alisema Mchinjita.
“Suala la SUK ni moja ya mambo ambayo kamati kuu itapokea taarifa yake na kutoa mwongozo. Kikao hicho pia kitafanya tathmini ya jumla ya masuala ya uchaguzi,” alisema.