ACT – Wazalendo yapendekeza hatua nne mchakato katiba mpya

Dar es Salaam. ACT Wazalendo imetangaza msimamo wake wa kuongoza mapambano ya kudai Katiba Mpya, ikisisitiza kuwa bila kuwa na Katiba Mpya, haki na demokrasia ya kweli haviwezi kupatikana nchini.

Akizungumza leo Jumatati Januari 19, 2026, kwa niaba ya chama hicho, Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita amesema Kamati Kuu ya chama imeazimia kutaka mchakato wa Katiba Mpya uanze mara moja ili kukidhi matakwa ya sasa ya wananchi.

“Kamati Kuu imeazimia kwamba ACT Wazalendo kitaongoza mapambano ya kupigania Katiba Mpya kwa sababu bila Katiba Mpya hakuna demokrasia wala haki. Tunataka mchakato huu uanze mara moja,” amesema Mchinjita.

Katika msimamo huo, ACT -Wazalendo imependekeza hatua nne muhimu zitakazotumika katika kuhuisha na kukamilisha mchakato huo nchini.

“Hatua ya kwanza ni kufanyiwa mapitio na marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 (Constitutional Review Act, 2011) pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2011 (Referendum Act, 2011), ili ziendane na mazingira ya sasa,” amesema makamu huyo.

Amesema chama hicho kimependekeza kuwa muswada wa kurekebisha sheria hizo uwasilishwe na kupitishwa katika mkutano wa Bunge unaoanza Januari hii.

Hatua ya pili Mchinjita amesema ni kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa wa wenye mamlaka, utakaowakutanisha wadau wote nchini kwa lengo la kujadili na kupata muafaka kuhusu masuala nyeti ya kikatiba ambayo bado hayajakubalika kwa pamoja, yakiwemo masuala ya Muundo wa Muungano.

Kwa mujibu wa ACT – Wazalendo, hatua ya tatu ni kuundwa kwa kamati ya wataalam wabobezi itakayokuwa na jukumu la kuandaa rasimu mpya ya katiba kwa kuzingatia maoni ya wananchi na makubaliano ya wadau.

“Hatua ya nne na ya mwisho ni kuitishwa kwa kura ya maoni, ili wananchi wawe na kauli ya mwisho ya kuamua kama wanakubali au wanakataa rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa,” amesema Mchinjita.

Amesema ACT – Wazalendo imesisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuwa shirikishi, huru na wenye uwazi, ili kuhakikisha katiba mpya itakayopatikana iwe inatokana na matakwa halisi ya wananchi na kulinda misingi ya demokrasia na haki nchini.