Bruce Melodie agonga kolabo na Diamond Platnumz


Na MWANDISHI WETU
MSANII wa muziki nchini Rwanda, Bruce Melodie ametoa kibao kikali kinachokwenda kwa jina la POM POM.

Katika wimbo huo, Bruce Melodie amepiga kolabo na wasanii wakali Afrika, Diamond Platnumz kutoka hapa Bongo na Joel Brown wa Nigeria.

Kazi hii iliyotolewa na 1:55 AM Entertainment, ni mchanganyiko wa Afro-pop, Bongo Flava na Afrobeats, ambapo inaunda wimbo mahiri wa Kiafrika ambao unaachia mchanyato wenye ladha ya aina yake.

POM POM ni kazi iliyosukwa na mikono ya prodyuza mkali kutoka nchini Ghana, C-Tea Beat, inayotoa burudani ya kipekee yenye mchanganyiko wa nchi tatu tofauti.

Kwenye wimbo huo unakutana na mashairi yenye lugha tatu – Kinyarwanda, Kiswahili na Kiingereza.

Akizungumzia kazi hiyo, Bruce Melodie amesema: “Ushirikiano huu unaadhimisha Afrika katika rangi zake zote – sauti tatu, nchi tatu, wimbo mmoja. ‘POM POM’ ni zaidi ya wimbo; ni harakati, ukumbusho kwamba muziki hutuunganisha bila kujali tunatoka wapi.”

Ukiachana na prodyuza C-Tea Beat, kuna mikono mingine mitatu imefanya kazi ya uongozaji katika video ya wimbo huo.

Vipande vyote vya Kigali, Rwanda amesimamia Fayzo Pro akishirikiana na Mganda Sasha Vybz (vipande vya Dar es Salaam, Tanzania), kazi inayotoa taswira ya tamaduni na utajiri wa majiji yote hayo.