Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema kabla ya kujiuzulu, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alikutana naye mara mbili kumweleza matatizo yake.
Kauli hiyo ya Butiku, inakuja ikiwa ni miezi mitatu tangu Polepole, alipochukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake eneo la Ununio, Dar es Salaam usiku wa Oktoba 6, 2025, tukio lililotokea miezi minne baada ya kujiuzulu ubalozi wa Cuba na kuanza kuikosoa Serikali na viongozi wake.
Baadaye Agosti 5, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wa Polepole na kumvua hadhi ya ubalozi.
Hata hivyo, Polepole mwenyewe katika moja ya video zake baada ya kujiuzulu amewahi kueleza kuwa kabla hajajiuzulu, alikutana na wazee kadhaa kuwaeleza changamoto zake na kuwaomba ushauri, ingawa hakuwataja majina.
Hatimaye leo, Jumatatu Januari 19, 2026, katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kikao cha wazee, Butiku ameweka wazi kuwa yeye ni miongoni mwa waliofuatwa na Polepole mara mbili kabla ya kujiuzulu.
Amesema mara ya kwanza, Polepole alimfuata na kumweleza changamoto zake za kazi alipokuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, kabla hajahamishiwa Cuba.
“Mara ya pili akaja akasema kusiwe na uchaguzi, nikamwambia kama hakuna uchaguzi hamtakuwa na Rais, kama huna Rais nani ataongoza nchi yenu, hatukukubaliana akaenda,” amesema.
Mara ya tatu, amesema hawakukutana bali alimpigia simu na kumweleza kwamba, kama ajenda ya kutofanyika uchaguzi haitakuwepo, anaona bora aache kazi (ya ubalozi wa Cuba).
“Nikamjibu fuata dhamiri yako. Asiniombe ruhusa kama anataka kuacha kazi, mimi sikumchagua, fuata dhamira yako, tangu wakati huo nilichomuona ni kwamba yuko kwenye mitandao, mwisho nimeona damu yake ni hii lakini mwenyewe sikumwona, mnajua aliko?” amehoji.
Hata hivyo, Butiku amesema ameona katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu wanadai anafahamu alipo Polepole, akisema hajui chochote, huku akilaani kitendo cha kutoweka kwake.
“Wako wengi (waliopotea), mmoja kijana mwenzenu Polepole (Humphrey) wanamtafuta mnajua aliko? Wanasema mimi najua, nataka kuwaambia leo sijui,” amesema Butiku.
Ameambatanisha hilo na kauli yake ya kukemea kupotea kwa watu, akisema ni ishara kwamba nchi imeshindwa kufuata utawala wa sheria.
Amesema kikao hicho cha wazee kinalenga kutafuta ukweli kwa kuwa wanaona Taifa limeanza kushindwa kuishi katika mfumo wa sheria, hivyo hakuna utawala wa sheria.
Amesema Katiba imeeleza Mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutoa uhai wa mtu tena kuna utaratibu wa kisheria.
“Nani ana ruhusa ya kwenda kuchukua mtu kwenye basi anatuaibisha kabisa kabisa, anamchukua mwenzetu anakwenda kuhakikisha ameuawa. Halafu kesho yake anakwenda kwenye mazishi kule Tanga anakwenda anatiririka …pale. Walimstahi walitakiwa wampige. Unatuletea maiti halafu unakuja kuhubiri dini hapa,” amesema.
Amesema haiwezekani kuwa na nchi ambayo raia wanapotea, wanaburutwa wanapotelea vichakani.
Sambamba na hayo, Butiku amesisitiza kutokana na yanayoendelea nchini na kile kilichotokea Oktoba 29, mwaka 2025, wazee wameona wafanye kikao kuujadili ukweli na kutafuta mwafaka.
Hata hivyo, amewataka Watanzania kuikubali tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza vurugu hizo, akisisitiza kama kuikataa, wasubiri wayakatae matokeo, sio tume yenye wajumbe mashuhuri na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo.
Katika mkutano wake huo, Butiku amesema kikao chao cha wazee kinalenga kujadili kwa kina sababu za vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka jana.
“Umoja wetu ulitikiswa siku hiyo, haikuishia hapo, walioongoza tunaambiwa walikuwa ni vijana wetu, watoto ambao wanatoka katika matumbo yetu.
“Wana mambo na sisi wazee, wakapigana, wakapambana na polisi. Wakachoma nyumba na nini na nini na Dar es Salaam ninyi mlikuwepo mliamrishwa mkae ndani watu zaidi ya milioni tano,” amesema.
Amesema kuna simulizi zinazodai kwamba waliotoka nje siku hiyo kwenda kununua mahitaji, walipigwa risasi.
“Mimi naamini katika utawala wa kijeshijeshi amri ukiipuuza kama kweli polisi waliona hatari ya kuchoma bandari na majengo mengine, unaweza kusema kama ni polisi hivi haya kaeni ndani, sitetei lakini nasema kilichotokea,” amesema.
Amesema tishio la kupigwa risasi ndilo lilifanya watu wakae ndani, isingekuwa hivyo wangelazimika kutoka nje kwa kuwa walikuwa na njaa na baadhi walikuwa na wagonjwa.
Butiku amesema nyumba yake ni miongoni mwa zilizopangwa kuchomwa moto akisema alipewa taarifa kuwa waandamanaji wanakwenda kwake, huku akiwa ndani.
“Wengine tuliletewa taarifa mimi ni mmoja wao, niliambiwa tunakuja kuchoma moto nyumba yako, iko mkoani Mara, nikasema mimi sijatoka nyumbani kwangu, vijana hawa wakanikuta, wakanibembeleza weee… watu wa usalama.
“Niliwauliza mnataka kunipeleka wapi, wakasema kwenda kukuficha na nani na wengine VIP, nikajiuliza kina nani Mkoa wa Mara huu, nikakataa waende kunificha labda hao wanaonificha nao ndio wananimaliza, nikawaambia huko siendi,” amesimulia Butiku.
Amesema aliwaambia atajificha mwenyewe na hakumwambia nduguye yeyote alikokwenda kwa kuwa aliambiwa nyumba yake itachomwa moto.
“Bunda (mkoani Mara) pale Ofisi ya TRA ilichomwa, nyumba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira imechomwa, nchi ikajaa askari polisi, kutishanatishana hivyo, uoga ukaingia, wakatoka TPDF kusaidia, wakabaki peke yao,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amesema baadaye viongozi walimfuata kumwomba kupitia Taasisi ya MNF, wasaidia kuleta umoja wa kitaifa kwa sababu wana jina la Mwalimu Nyerere.
Butiku ameeleza changamoto nyingi za utawala wa sheria zinazoshuhudiwa, msingi wake ni Katiba ambayo kwa kipindi kirefu imeshindikana kufanyiwa mabadiliko.
Lakini, amesema kuna matumaini ya hilo kutokea hasa baada ya mkuu wa nchi wa sasa (Rais Samia), kuahidi kuanza kulifanyia kazi hilo ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.