GOLI alilofunga jana mshambuliaji wa Al Nassr ya Saudia, Clara Luvanga dhidi ya Neom SC Ligi Kuu ya wanawake ya Saudi Arabia limemfanya afikishe idadi ya mabao 12 na asisti tatu na kukaa kileleni mwa wafungaji bora.
Huu ni msimu wa tatu wa Clara Saudia, wa kwanza alifunga mabao 11 na asisti saba, uliofuata aliweka kambani mabao 21 na asisti saba na msimu huu ikiwa raundi ya saba amefunga mabao 12 na asisti tatu.
Idadi ya mabao aliyofikisha imemfanya aivunje rekodi ya msimu wake kwanza kuitumikia Al Nassr na kama ataendelea kupata nafasi ya kufunga huenda akaivunja rekodi ya msimu uliopita.
Akizungumzia kiwango hicho Clara amesema; “Nimejiwekea malengo msimu huu nje ya timu basi angalau nichukue kiatu cha ufungaji bora wa ligi ingawa nilichukua kwenye mashindano ya Challenge Cup lakini lengo langu halijatimia.”
Mbali na Clara wachezaji wengine wa Kitanzania waliokuwa kibaruani wiki hii, Chama la Opah Clement Eibar lilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Madrid CFF katika mwendelezo wa Ligi ya Wanawake Hispania, nahodha huyo wa Twiga Stars aliingia dakika ya 75.
Watanzania wengine wawili wanaokipiga Ligi ya Misri, Hasnath Ubamba alimaliza dakika 90 dhidi ya Zamalek walipoondoka na ushindi wa mabao 4-0 na mwenzie Violeth Nickolaus akianzia benchi.