Depu aanza kazi, Yanga ikiichapa Mashujaa

Nyota mpya wa Yanga, Laurindo Aurelio ‘Depu’ ameanza kwa neema ndani ya klabu hiyo baada ya leo kuhusika na mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-0 ambao timu yake imeupata dhidi ya Mashujaa FC, katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Nyota huyo raia wa Angola, amefunga bao moja na kupiga pasi moja ya mwisho akiiwezesha Yanga kupata ushindi huo ambao umeipeleka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Depu aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Maxi Nzengeli, alianza kwa kupiga pasi iliyozaa bao la Mudathir Yahya katika dakika ya 81.

Dakika ya 89, Depu aliwainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kuifungia timu hiyo bao la sita akimalizia mpira uliotemwa na kipa Erick Johora baada ya mkwaju wa faulo wa Allan Okello.

Katika mechi hiyo ya leo, mabao mengine ya Yanga yamefungwa na Prince Dube, Mohamed Damaro, Duke Abuya na Pacome Zouzou.

Baada ya dakika 90 kukamilika, Mudathir Yahya alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Kipa wa Yanga, Abuutwalib Mshery aliondoka mifuko ikiwa imenona baada ya kutuzwa fedha na kundi kubwa la mashabiki wa Yanga walioonekana kukoshwa na kitendo cha kipa huyo kumaliza mchezo bila kuruhusu bao (clean sheet).

Huo ni ushindi wa sita kati ya saba iliyocheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambapo imepanda rasmi kileleni ikifikisha pointi 19, mbili zaidi ya zile za JKT Tanzania iliyokuwa ikiongoza hapo awali.

Baada ya ushindi huo, kibarua kinachofuata kwa Yanga hivi sasa ni mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huko Cairo, Misri, Ijumaa wiki hii dhidi ya Al Ahly.