Gofu yakusanya Sh112 milioni za kutibu macho

MASHINDANO Maalumu ya Gofu ya Dar es Salaam Mzizima ‘Lions play for Sight’ yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana yakishirikisha wachezaji 70, yamekusanya jumla ya Sh112 milioni, zitakazotumika katika kuchangia huduma ya macho.

Mratibu wa mashindano hayo, Ragib Hassanali amesema wachezaji hao wanatoka klabu za gofu za Lugalo, Morogoro Gymkhana  na Dar es Salaam Gymkhana na fedha hizo zitatumika kutoa huduma za macho kwa watu zaidi ya 50,000 zikiwemo shule 36 za Mkoa wa Dar es Salaam.

“Mbali na hilo, kilichopatikana kitakwenda kusaidia pia wenye tatizo la mtoto wa jicho kwa watu 500,” amesema Hassanali.

Mratibu huyo pia amesema kutokana na kuwepo kwa maombi mengi, ifikipo Machi mwaka huu,  wanatarajia kwenda kutoa huduma hizo pia Wilaya ya Bariadi, iliyopo mkoani Simiyu. 

Katika  mashindano hayo Lions Plays for Sight, mchezaji Son Vengtsamy aliibuka mshindi wa jumla kwa pointi 40, akifuatiwa na Rustom Somji aliyepata pointi 37.

Upande wa Divisheni A, nafasi ya kwanza ilichukuliwa Abid Omary aliyepata pointi 37 akifuatiwa na Peter Fiwa aliyepata pointi 36.

Upande Divisheni B, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Pareshi Patel aliyeshinda kwa pointi 40 huku Ali Timimu akishika nafasi ya pili kwa pointi 34 na kwa upande wa Division C kinara alikuwa ni Thabit Galia aliyepata pointi 34, akifuatiwa Ajay Sha aliyepata pointi 33.

Kwa upande wanawake Timea Chogo alishinda kwa pointi 28, akifuatiwa na Anita Siwale aliyepata pointi 24, huku kwa upande wa upigaji wa mpira wa mipira ya mbali ‘Longest Drive’ upande wanawake ilichukuliwa Timea Chogo na wanaume ni Peter Fiwa.

Aidha Mohamed Assgarali alishinda upande wa wanaume kwa mpira uliofika karibu na shimo (Nearest to the pin) na wanawake alikuwa ni Ruth Maweo.