Hatua za kupunguza foleni mpakani Tunduma zaanza

Dar es Salaam. Agizo la Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuvunjwa ukuta uliopo pembezoni mwa barabara ya Tunduma ili ipatikane nafasi ya kupanua barabara hiyo, utekelezaji umeanza.

Kauli hiyo ya kuanza kwa utekelezaji wa agizo hilo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame alipozungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 19, 2025 kwa simu.

Desemba 17, 2025 Dk Mwigulu alitoa agizo hilo akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Songwe akisema  ameshazungumza na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda kuhusiana na kuvunjwa kwa ukuta huo ili kupisha hatua ya kutanua barabara.

Makame amesema baada ya maelekezo ya Waziri Mkuu, tayari zipo hatua zilizoanza kuchukuliwa kuhakikisha tatizo la foleni katika Mji wa Tunduma linaisha.

Amesema baadhi ya hatua ni pamoja na kukaa vikao vya mara kwa mara vinavyohusisha wadau na taasisi mbalimbali ikiwamo wizara, taasisi na mamlaka zinazohusika na miundombinu ambayo itasaidia kuwezesha kukamilika kwa miradi, itaweza kumaliza foleni hiyo.

“Utekelezaji unaridhisha na Serikali kama ilivyoahidi kuhakikisha changamoto ya foleni inaisha, tumejipanga kusimamia vizuri ili kufikia malengo na wananchi waendelee kuamini tatizo litaisha,” amesema Makame.

Kwa upande wake Kamishna wa TRA, Mwenda akizungumzia agizo hilo la Waziri Mkuu amesema tayari wamesharuhusu na wametuma timu ya wataalamu mkoani Songwe kwa ajili ya kazi hiyo.

“Kwa sisi TRA tumesharuhusu na tayari kuna wataalamu kule, tumeacha wataalamu wakituambia chochote kinafanyika tu,” amesema kamishna huyo.

Barabara hiyo inayobeba uchumi wa Mkoa wa Songwe, imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara kutokana na msongamano wa malori yanayoingia na kutoka nchini.

Kutokana na kilio hicho cha foleni katika eneo hilo la Tunduma, yaliwahi kutolewa maagizo na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega Desemba 13,2025 ambaye pia aliuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kufanya tathmini ya kutanua barabara katika mpaka wa Tunduma.

Barabara hiyo pia inapitisha magari yaendayo nchi jirani za Zambia na Congo.

Waziri Ulega alitoa agizo hilo akiwa Tunduma mkoani Songwe na kueleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanayopitia wasafirishaji na wananchi wa eneo hilo kutokana na msongamano wa malori kwa muda mrefu.

 “Namuagiza Mkurugenzi kutoka Tanroads watafute fedha haraka ya dharura, pafanyike tathmini na tutapanua hapa mara moja ili zile njia tatu zijengwe hapa na kupunguza msongamano uliopo wa malori eneo hili,” alisema.