KOHE MATATANI KWA UVAMIZI WA BENKI SIRARI NA KUTAKA KUPORA SILAHA KWA POLISI

::::::::::

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/ Rorya kupitia kwa Kamanda wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mark Njera ameseme picha Mjongeo inayosambazwa Mtandaoni ikimuonesha Askari Polisi akipambana na mtu mmoja, imetokana na tukio la mtu huyo (John Kohe Amos) kuvamia Benki ya CRDB tawi la Sirari na kuamuru kupewa fedha bila kufuata taratibu.

Kamanda Njera katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Januari 19, 2025 amesema katika tukio hilo la Januari 15,2026, Mtu huyo Mkazi wa Kijiji cha Sokoni– Sirari, alifika katika benki hiyo saa nane mchana na kuingia ndani na kwenda kwa mtoa huduma wa benki (bankteller) kama mteja huku akiwa amebeba begi dogo na kumwamuru kwa nguvu mtoa huduma ampe fedha bila kufuata taratibu za kibenki.

Taarifa ya Polisi imesema hali hiyo ilisababisha wasiwasi ndani ya Benki hiyo na kulazimu Askari Polisi waliokuwa lindo nje ya Benki hiyo kuitwa na baadae kumfuata mtu huyo na kumtaka atoke nje, suala ambalo alitii na walipofika nje akafanya jaribio la kumnyang’anya Askari Polisi silaha yake ya moto ili kupambana naye.

“Wakati anasindikizwa na Askari kutoka nje ghafla alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha kwa kupambana na askari, hata hivyo askari walifanikiwa kumdhibiti na kumtoa nje ya benki bila kutumia silaha pamoja na kitendo alichofanya.” Amesema Kamanda Njera.

Kulingana na Polisi, uchunguzi pia umebaini kuwa mtu huyo hakuwahi kuwa Mteja wa Benki hiyo wala kuwa na Akaunti, ambapo kwasasa uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini nia ya mtu huyo na kile kilichokuwa kinamsukuma kufanya tukio hilo ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuata.