Londo ahimiza bunifu za kiteknolojia kuchochea mapinduzi ya kilimo

Arusha. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amezitaka taasisi za utafiti na ubunifu wa zana za kilimo nchini kubuni na kuendeleza teknolojia za kisasa zitakazobadilisha kilimo cha jadi na kukifanya kiwe chenye tija, shindani na kusaidia nchi kufikia uchumi wa trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Londo ameyasema hayo leo Januari 19, 2026 wakati akizungumza na wataalamu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec) katika ziara yake ya siku moja jijini Arusha.

Amesema kuwa maendeleo ya kilimo ndiyo msingi wa maendeleo ya viwanda na chanzo kikuu cha malighafi za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na kukuza biashara na uchumi wa Taifa, hivyo bunifu ndio itakayosaidia wakulima kupiga hatua.


Amesema kuimarishwa kwa kilimo na kuwa chenye tija kutaiwezesha sekta ya viwanda na biashara kuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja.

“Tanzania haina budi kuwekeza kwa nguvu katika bunifu za zana za kilimo ili kujenga uchumi jumuishi unaomshirikisha kila mwananchi, hususan wakulima walioko vijijini.

“Dira ya 2050 inalenga uchumi shindani, himilivu na jumuishi, ambapo sekta ya viwanda ni mhimili mkuu, lakini kwa nchi inayoendelea kama Tanzania, viwanda vina uhusiano wa moja kwa moja na kilimo chenye tija na nyie ndio tunaowategemea kuongoza katika hili,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Ukisema uzalishaji katika nchi kama Tanzania, moja kwa moja unazungumzia kilimo, bado tuna safari ndefu mbele kwa sababu kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wetu, kuanzia Dira ya 2025 hadi 2050,” amesema.

Londo amesema anasikitishwa na hali ya wakulima wengi kuendelea kutumia jembe la mkono katika karne ya sasa, kwani hali hiyo haiendani na azma ya kumtoa mkulima katika umaskini na kumpa maisha bora.


“Binafsi naumia kuona mkulima anatumia jembe la mkono leo, wakati hata walinzi wa wanyama hawakubali ng’ombe akokote jembe kwa sababu ni mateso. Haya yote hayaendani na ndoto yetu ya kumuinua mkulima,” amesema.

Kwa mujibu wa Londo, matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali katika kilimo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, kupunguza muda wa kazi, kuongeza kipato cha mkulima na kuchochea uchumi wa vijijini kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Camartec, Godfrey Mwanama amesema kituo hicho kinaendelea kuandaa majibu ya changamoto za ajira na uchumi kwa kubuni zana za kilimo zenye tija na zinazokidhi mahitaji ya wakulima.

Amesema Camartec imeanzisha mpango wa viwanda darasa, unaolenga kubaini mahitaji halisi ya zana za kilimo kwa ajili ya kuzizalisha, sambamba na kuwajengea wananchi uelewa wa teknolojia zilizopo na namna ya kuzitumia.

“Tumegundua kuwa kuna teknolojia nyingi nchini, lakini wananchi hawajui zinatumikaje, ndiyo maana tumeanzisha viwanda darasa ili kuongeza uelewa na matumizi ya teknolojia hizo,” amsema Mwanama.

Ameongeza kuwa Camartec inaelekea kuwekeza katika bunifu za zana zinazotumika katika uchumi wa buluu, hususan kwa usindikaji wa mazao ya mwani, dagaa na samaki. 

Pia, amesema kituo hicho kinaangalia fursa za kusindika matunda kama parachichi, machungwa na maembe wakati wa msimu wa uzalishaji mkubwa, ili kupunguza upotevu wa mazao, kuongeza thamani na kuinua kipato cha wakulima.

Katika ziara hiyo, Londo ametembelea pia Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (Temdo).