Mido Msauzi mwenye mambo mawili asubiriwa Simba

KAMA ulikuwa unadhani mabosi wa Simba wamelala katika dirisha dogo la usajili lililo wazi kwa sasa, basi pole yako.

Unaambiwa mabosi wa klabu hiyo wanaifanya kazi yao kimyakimya kwa sasa bila kutaka kuwashtua wapinzani na kitakachofuata ni sapraizi ya bandika bandua tu kwa mashabiki.

Ndiyo. Inadaiwa hadi sasa Simba tayari imekamilisha dili nne matata za nyota wa kigeni kutoka mataifa tofauti na imeanza kuwatambulisha mmoja baada ya mwingine ikianza na winga kutoka Senegal, Libasse Guaye, lakini kwa sasa ipo hatua nzuri kushusha kiungo mwingine fundi wa mpira raia wa Afrika Kusini ikiwa ni pendekezo la kocha mkuu, Steve Barker anayetokea huko pia.

Mido hiyo ya boli ni Genino Tyrell Palace mwenye umri wa miaka 27 kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini na inadaiwa mazungumzo yamefikia pazuri na lolote linaweza likatokea.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba, kimeliambia Mwanaspoti, kocha Barker aliyetokea katika klabu hiyo na aliyekuwa akimnoa Genino, alipewa nafasi ya kuwaangalia wachezaji wa Msimbazi kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi kisha atoe tamthmini yake.

Ndipo kocha huyo aliyeifikisha Stellenbosch nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ikitolewa na Simba iliyocheza fainali na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa mabao 3-1, alitoa mapendekezo kwa kulipeleka jina la kiungo huyo mezani kwa mabosi wa Simba akiwaambia ‘Mleteni huyu jamaa tupige naye kazi hapa’.

Barker aliwapa sifa za mido huyo ni uwezo wa kucheza kama kiungo mkabaji na pia kiungo mshambuliaji akiamini atafukia mashimo aliyoyaona kupitia michuano ya Mapinduzi kwa kikosi cha Simba kilichotolewa nusu fainali kwa kufungwa bao 1-0 na Azam FC.

“Genino ana mkataba na timu ya Stellenbosch ndiyo maana viongozi wanazungumza hilo na makubaliano yanakwenda vizuri, ukiachana na huyo kuna wachezaji wa kigeni ambao mazungumzo yanaendelea,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kabla ya kocha kujiunga na timu wapo wachezaji wa kigeni ambao viongozi walipanga kuachana nao kama (Neo) Maema, (Joshua) Mutale na (Steven) Mukwala lakini kocha ana mapendekezo yake ya nani atoke nani aingie.”

Chanzo hicho kilisema sababu ya kocha kumhitaji Palace aliyezaliwa Desemba 19, 1998 ni uwezo wake wa kunyumbulika akikaba na kushambulia.

“Baada ya kulileta jina lake viongozi walifuatilia baadhi ya mechi alizocheza wakajiridhisha na kuona anaweza akaongeza nguvu katika timu,” kilisema chanzo hicho.

Endapo kama dili la Genino litafanikiwa, basi idadi ya wachezaji wanatajwa kufyekwa Msimbazi itaongezeka, kwani tayari kuna mashine nyingine nne za kimataifa zinatajwa zimeshakamilisha usajili Msimbazi na kilichobaki ni kutangazwa tu kuanzia sasa.

Inadaiwa Simba imeshamnasa kipa mpya kutoka Niger, Mahamadou Tanja, beki wa kati raia wa DR Congo, Ndongani Samba Gilbani kutoka Asante Kotoko ya Ghana, pia kuna beki wa kushoto raia wa Mauritania, Khadim Diaw aliyekuwa akihusishwa tangu dirisha kubwa la usajili msimu huu.

Lakini kuna nyota mwingine ambaye jina lake limekuwa gumu kutajwa kutoka klabu ya AS Maniema ya DR Congo, huku tayari Jean Charles Ahoua akiwa ameshauzwa kwenda CR Belouizdad ya Algeria na kutoa nafasi kwa nyota wapya kuingia na wengine wakipigiwa hesabu kufyekwa.

Katika orodha ya sasa, wachezaji wanaotajwa huenda wakaachana na Simba ni Joshua Mutale ambaye msimu wa 2024-2025 katika Ligi Kuu Bara alimaliza na asisti mbili bila bao na 2025-2026 akipiga asisti moja, hajafunga. Mwingine ni Steven Mukwala ambaye msimu wa 2024-2025 alifunga mabao 13 na asisti tatu, huku msimu huu 2025-2026 hajafunga ila ana asisti moja. Pia Neo Maema na beki wa kati Chamou Karaboue wanaopigiwa hesabu kutolewa kwa mkopo klabu nyingine.

Baadhi ya nyota wa zamani wa Simba walikuwa na maoni baada ya uwepo kwa taarifa za usajili mpya wa klabu hiyo ambapo Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amesema: “Pamoja na usajili unaofanywa mabadiliko makubwa yanatakiwa kufanyika ili kujua kipi kimewakwamisha kushindwa kuchukua misimu minne mfululizo, kama ni kusajili wamesajili sana na kuacha makocha.”

Mkongwe mwingine wa klabu hiyo ni Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ amesema: “Uongozi ukitulia kila kitu kitakwenda sawa na malengo ya klabu yatatimia nje na hapo bado kunaweza kukawa na changamoto, msimu uliomalizika Simba ilisajili sana lakini bado ubingwa ukakosekana.”

Simba leo itashuka kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuvaana na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu kabla ya kusafiri hadi Tunisia, kukabiliana na Esperance kwa pambano la Kundi D la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Januari 24, 2026.

Simba itarudiana na Esperance Januari 30, 2026 katika kusaka pointi za kufufua tumaini la kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwani awali ilipoteza mechi mbili za kundi hilo mbele ya Petro Atletico ya Angola iliyowalaza 1-0 nyumbani na kupoteza pia 2-1 ugenini kwa Stade Malien ya Mali na kuifanya timu hiyo ishike mkia wa kundi hilo.