:::::::::::
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewaelekeza Wasimamizi wa Miradi wa Mikoa kuhakikisha wanaimarisha Mawasiliano na Ushirikiano na wadau mbalimbali kwenye maeneo ya miradi ili kurahisisha utekelezaji wake.
Ametoa maelekezo hayo leo Januari 19, 2026 jijini Dodoma katika kikao chake na Watumishi wa REA wanaohusika na Usimamizi wa Miradi wa Mikoa mara baada ya Kusaini mikataba ya kusambaza umeme katika Vitongoji 9,009 Tanzania Bara.
“Tarehe 17 Januari, 2026 tulisaini mikataba na Wakandarasi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 9,009 na tunaelekea kwenye hatua ya utekelezaji, nimewaiteni hapa ili tukumbushane namna bora ya kuimarisha utendajikazi wetu,” amesisitiza Mha. Saidy.
Amesema Watanzania wanayo matumaini na REA na kwamba ni wajibu wao kuhakikisha hawawaangushi kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Miongozo ya Serikali.
“Imarisheni mawasiliano na ushirikiano na Wabunge, Viongozi wa Mikoa, Wilaya, TANESCO, Wakandarasi, Serikali za Vijiji na Vitongoji pamoja na wanufaika wa miradi,” amesisitiza Mha. Saidy
Halikadhalika Mha. Saidy amewasisitiza kuendelea kuwasimamia kwa karibu Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nishati vijijini ikiwemo kuwa na ratiba yao ya kila siku na kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi katika ngazi mbalimbali kuanzia vitongoji hadi ngazi ya mkoa ili kuwapa nafasi ya kutambua hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi.
“Hakikisheni mkandarasi anaripoti kwenye uongozi wa kitongoji kabla hajaanza kutekeleza kazi yoyote ya mradi na pia msisitize katika suala la kutoa ajira kwa wananchi eneo la mradi,” ameelekeza Mha. Saidy.
Vilevile amewataka kuhakikisha wanawasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi kwa viongozi huko walipo kwenye maeneo yao ya miradi ili iweze kujulikana na namna inavyoendelea kutekelezwa ikiwepo kutambua changamoto zilizopo na kuzitafutia suluhisho mapema.
Pia, amewasisitiza kushirikiana na Taasisi zingine za Serikali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hasa ikizingatiwa kuwa mradi unapitia hatua mbalimbali za utekelezaji na Kila hatua inakuwa inahitaji ushirikiano na wadau wengine zikiwemo baadhi ya taasisi zinazotekeleza miradi ya maendeleo maeneo ya vitongoji ikiwemo TARURA na TFS.
Kikao hicho kicho kimelenga kujadili namna bora ya kusimamia utekelezaji wa miradi, hatua zilizofikiwa na mikakati ya kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kasi ili ikamilike ndani ya muda.


