Songea. Victor Mhagama, mtoto wa marehemu Jenista Mhagama, amejitosa kuwania kurithi nafasi ya ubunge ya Peramiho iliyoshikiliwa na mama yake kwa zaidi ya miaka 20 kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hatua hiyo inamfanya Victor kuingia katika orodha ya watoto wa vigogo kadhaa wa siasa ndani ya chama hicho waliojitosa kuwania kurithi majimbo ya wazazi wao waliopofariki dunia.
Miongoni mwa watoto hao, yumo Omar Kigoda, aliyewahi kuchukua fomu kuwania ubunge wa Handeni, baada ya baba yake, Abdallah Kigoda, kufariki dunia akiwa mbunge wa jimbo hilo.
Mwingine ni Goodluck Mtinga, mtoto wa kwanza wa marehemu Celina Kombani, aliyewania ubunge wa jimbo la Ulanga Mashariki, baada ya kifo cha mama yake akiwa na wadhifa huo.
Vivyo hivyo, ilitokea kwa Geofrey Mgimwa, mtoto wa Dk William Mgimwa, aliyewania ubunge wa Kalenga baada ya baba yake kufariki dunia akiliongoza jimbo hilo.
Aidha, Salum Turky naye alijitosa kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo, baada ya baba yake, Turkey Taufiq, aliyekuwa Mbunge wa Mpendae, kufariki dunia.
Hata hivyo, Victor atachuana na makada wengine watano wa CCM, wakiwamo viongozi wa chama hicho Songea Vijijini, waliojitosa kuwania kuteuliwa kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Dalili za uamuzi wa Victor kuwania nafasi hiyo ya kumrithi mama yake, zilionekana tangu siku ya ibada ya kuaga mwili wake iliyofanyika mkoani Ruvuma.
Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alimpigia chapuo ingawa kwa mafumbo. “Mkuu wa mkoa uko hapa, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi upo hapa, na nyota mtoto wetu (Victor) yupo hapa. Nafikiri nikisema hivyo mmenielewa. Mmenielewa?” alisema Zungu.
Kufanyika kwa mchakato huo wa uchukuaji na urejeshaji fomu katika jimbo hilo kunatokana na kubaki wazi kwa nafasi ya ubunge wa Peramiho tangu Jenista alipofariki dunia Desemba 11, mwaka jana.
Akizungumzia hilo leo Jumapili, Januari 18, 2026, Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Juma Nambaila, amesema uchukuaji na urejeshaji fomu umeanza leo Jumapili, Januari 18, na utafungwa kesho, Jumatatu, Januari 19.
Amewataja waliochukua fomu pamoja na Victor ni Emilly Ngaponda, Scholar Ngonyani, Clemence Makaburi, Allen Mhagama na Rosemery Mashauri.
Amewataka wanachama wenye sifa na nia ya kugombea kuzingatia maelekezo ya chama na kuhakikisha fomu zinarejeshwa ndani ya muda uliopangwa.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Schoral Daniel, amesema anaamini ana uzoefu kwenye uongozi.
Amesema analijua vema jimbo hilo kwa kuwa alishirikiana na Jenista kutatua kero za wananchi wa Peramiho, na hivyo anaamini atakuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto zao kwa ufanisi.