Mukwala asepa, aibukia Uarabuni | Mwanaspoti

KAMA Mwanaspoti lilivyowajulisha mapema baada ya Jean Charles Ahoua kuuzwa CR Belouizdad ya Algeria, pia Steven Mukwala naye alikuwa mbioni kuondoka klabuni hapo, ndivyo ilivyo kwa sasa baada ya straika huyo raia wa Uganda kutua Al-Nasr ya Libya.

Licha ya Mukwala jana  kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba ilibanwa nyumbani na kutoka sare ya bao 1-1, lakini ukweli hakuwa katika mipango ya timu hiyo, kwani mabosi walikuwa wanamtafutia timu ya kumpeleka kwa mkopo.

Nyota huyo ambaye alibakiza miezi sita kumaliza mkataba wake wa miaka miwili aliosaini wakati anatua Julai 2024 akitokea Asante Kotoko ya Ghana, ametua Al-Nasr na hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba alichokitumikia tangu msimu uliopita na kukifungia mabao 13 katika Ligi Kuu Bara, timu hiyo ikimaliza nafasi ya pili nyuma ya Yanga.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba, kililiambia Mwanaspoti wamefanya biashara ya kumuuza mshambuliaji huyo ambaye ofa yake imetua mapema mwezi huu.

“Ni kweli Mukwala alikuwa sehemu ya wachezaji ambao walitakiwa kupisha usajili mpya ndani ya timu yetu kutokana na benchi jipya la ufundi kushindwa kukubaliana na uwezo wake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Baada ya biashara kufanyika sasa bado nafasi ya wachezaji wengine wawili ambao pia kocha amesema hawahitaji kikosini na kuomba kuongezewa wachezaji wengine bora watakaoendana na mpango wake.”

Chanzo hicho kilisema wanapambana kusuka kikosi chao kutokana na kasoro zilizoonekana na wanaamini bado wana nafasi ya kufanya vizuri na kurudi kwenye ushindani.

Mukwala msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Simba 2024-2025 alifunga mabao 13 na asisti tatu akiwa na mchango wa mabao 16 akicheza dakika 1171.

Kutimka kwa Mukwala ndani ya kikosi hicho, atakuwa mchezaji wa pili kuuzwa kipindi hiki cha dirisha dogo baada ya Jean Charles Ahoua aliyetua CR Belouzdad, huku klabu hiyo ikiwa imeshamsajili Libasse Gueye kutoka Senegal na ikielezwa imemalizana na Genino Palace kutoka Afrika Kusini. Wengine waliotolewa kwa mkopo ni Awesu Awesu aliyekwenda Kenya Police na Mzamiru Yassin aliyetua Mashujaa.

Kwa sasa Simba inajiandaa na mechi ngumu za Kundi D kunako Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia ikianzia ugenini Jumamosi hii, kisha kurudiana jijini Dar, Januari 30, 2026.

Simba inayoburuza mkia wa kundi hilo baada ya kupoteza mechi mbili dhidi ya Petro Atletico ya Angola (1-0) na Stade Malien kutoka Mali (2-1), kwa sasa inanolewa na kocha mpya, Steve Barker aliyetua kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini.