Mzee: Chadema ndio chama halisi cha upinzani

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Said Mzee amesema kutokana na misingi ya chama hicho, hakuna mtu anayeweza kukinyooshea kidole kwamba kinafungamana na chama kingine cha siasa.

Amesema hakuna mtu anayeweza kusema Chadema ni CCM B, washirika wa ACT Wazalendo au Chama cha Wananchi (CUF).

Mzee ametoa kauli hiyo leo Januari 19, 2026 kupitia mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa na Baraza la Wazee Chadema (Bazecha) ukijikita kuelezea historia ya Chadema upande wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 33 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

“Hiki ni chama kinachojitegemea na kinasimama kwa miguu yake na kinaaminiwa na Wazanzibar wote na kuwa ni chama halisi cha upinzani,” amesema.

Kutokana na imani hiyo, amesema matumaini ya chama hicho kushika dola zinakaribia na ana imani uchaguzi 2030 yapo mambo makubwa yatakayotokea kupitia chama hicho.

Akizungumzia Bazecha, amesema limekuwa nguzo muhimu ya kutatua migogoro lakini kimesaidia kuiweka Chadema salama.

Amesema miaka ya nyuma walikuwa wanahangaika kutafuta wazee ndani ya Chadema lakini sasa hali imekuwa tofauti kutokana na watu wengi kukiamini chama hicho.

“Ukiangalia sasa baraza letu lina uongozi kuanzia ngazi ya msingi, tawi, wodi, jimbo, wilaya hadi Taifa, tuna viongozi ambao wana umri wa kikatiba, nilipongeze pia baraza kwa kufanya kongamano kubwa hapa Zanzibar mwaka 2015,”amesema.

Amesema vijana wa zamani walioanzisha chama ndio wazee wa sasa ndani ya chama na hata mahakama ya wanachama wanaounga mkono juhudi kutoka kundi la vijana.

Amewataka viongozi kuondokana na zana kwamba baraza hilo sio la kutuliza tu migogoro bali wachukue jukumu kuongoza chama kushika dola.

“Ninaamini tukitumia jukwaa la wazee, mabadiliko katika nchi yetu yatapatikana,” amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Bazecha, Hellen Kayanza amesema Chadema ina baraza la wazee na kazi yake kubwa ni kutatua migogoro.

“Chama kiliona kwa umakini kabisa, kuna migogoro na kutoelewana, hivyo chama kikaona umuhimu wa kuanzishwa kwa baraza la wazee kusuluhisha,” amesema.

Amesema mbali na jukumu hilo, kazi nyingine waliyonayo ni kukijenga chama.

Katibu Mkuu huyo amesema ana uhakika Chadema inapoelekea inakwenda pazuri na sasa chama hicho kimekuwa taasisi kubwa, hakiwezi kurudi nyuma.

“Tunashukuru Watanzania wametuamini tumefikia hapa, hili ni jambo kubwa la kumshukuru Mungu, hili ni jambo la kujipongeza na mimi sijutii kuwa Chadema kwa sababu sasa hivi ipo chati ya juu na huko mbele mafanikio ni ya juu sana, ”amesema.