Richardson Ng’ondya atua anga za KMC

KMC inaendelea na maboresho mbalimbali dirisha hili dogo na kwa sasa uongozi wa kikosi hicho uko katika mazungumzo ya kumnasa kiungo mshambuliaji wa Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, Richardson Ng’ondya.

Nyota huyo wa zamani wa Mbeya City na Kagera Sugar, ni pendekezo la benchi la ufundi la kikosi hicho chini ya kocha mkuu wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, ambaye ameonyesha nia ya kumhitaji ili akaongezee nguvu eneo la ushambuliaji.

Taarifa kutoka uongozi wa KMC, umeliambia Mwanaspoti wawakilishi wa mchezaji huyo wanafanya mazungumzo hayo kwa ajili ya kuipata saini ya Ng’ondya, ambaye kwa sasa amebakisha mkataba wa miezi sita tu na kikosi hicho cha Geita Gold.

Hata hivyo, licha ya KMC kuonyesha uhitaji wa nyota huyo, ila Mwanaspoti linatambua Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila, ameutaka uongozi wa timu hiyo kuhakikisha haimruhusu mchezaji yeyote muhimu kuondoka kwa sasa katika dirisha hili dogo.

“Malengo ya Geita Gold ni kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, sasa ikiwa tutaruhusu wachezaji bora waondoke kirahisi maana yake tunajiweka mbali na kile tunachokipambania, ndio maana kocha ameweka msisitizo hilo,” kilisema chanzo hicho.

Mbali na Ng’ondya, nyota wengine wanaokaribia kujiunga na KMC ni beki wa kati, Mudathir Nassor Ally kutoka Zimamoto FC na kiungo, Suleiman Juma Kidawa ‘Pogba’ aliyekuwa Mlandege, ambapo nyota wote hao wawili wanatokea visiwani Zanzibar.

Wengine ni kiungo, George Sangija aliyetamba na Mbao, Geita Gold, Mbeya City, Tanzania Prisons na KenGold na John Tibar aliyezichezea Ndanda, Singida United, MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech, FC Baniyas na Hatta Club zote za Falme za Kiarabu.