Dar es Salaam. Serikali imetangaza mkakati mpana wa kuharakisha uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, ikilenga kuiweka nchi kama kitovu cha kikanda na Bara la Afrika katika uzalishaji wa dawa zenye viwango vya kimataifa.
Hatua hiyo imekuja sambamba na ahadi ya ulinzi wa soko kwa wazalishaji wa ndani watakaokidhi viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Inaelezwa awali kuwa changamoto kubwa iliyokwamisha viwanda vya ndani vya dawa ilikuwa ni kushindwa kufikia viwango vya kimataifa vya uzalishaji, hususan vinavyotambuliwa na WHO na Good Manufacturing Practice (GMP).
Akizungumza leo Jumatatu, Januari 19, 2026, katika Jukwaa la Kimkakati la Uwekezaji wa Bidhaa za Afya Tanzania, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema Serikali imeamua kuondoa utegemezi mkubwa wa dawa zinazoagizwa kutoka nje, akisisitiza kuwa usalama wa afya ya taifa hauwezi kujengwa kwa uagizaji pekee.
Amesema Serikali imeanzisha Mkakati wa Kuharakisha Sekta ya Dawa (Pharmaceutical Acceleration Strategy) unaolenga kuondoa urasimu na kucheleweshwa kwa maamuzi ya uwekezaji.
Chini ya mkakati huo, utaratibu wa leseni, vibali, ardhi, kodi, usajili wa bidhaa na miundombinu zitashughulikiwa kwa wakati mmoja badala ya kimoja kimoja, hatua inayotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kuanzisha viwanda hivyo.
Ili kusimamia utekelezaji wake, Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (PIAT), chenye mamlaka ya moja kwa moja ya kuratibu na kutoa uamuzi wa haraka kuhusu uwekezaji wa kimkakati.
Kikosi hicho kinawakutanisha wawakilishi wa sekta za sera, fedha, ardhi, nishati, biashara, udhibiti na ununuzi wa umma, lengo likiwa kuondoa vikwazo vya kimuundo vilivyokuwa vikiathiri wawekezaji.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa ametangaza rasmi Tangazo la Nia (Expression of Interest – EOI) kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa kuwekeza katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya.
“Tangazo hili linahusisha pia kuhimiza ushirikiano kati ya wazalishaji wa ndani na kampuni za kimataifa, pamoja na kuvutia mtaji, teknolojia na masoko ya nje. Mwisho wa kuwasilisha maombi haya itakuwa Machi 2, 2026,” amesema.
Ameeleza lengo kuu la mkakati huo ni kujenga mamlaka ya afya ya taifa, kuiweka Tanzania kama mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa dawa barani Afrika, pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa dawa za kisasa zinazojulikana kama ‘advanced generics’.
Mchengerwa amesema dawa nyingi zinazotumika barani Afrika bado zinategemea teknolojia zilizopitwa na wakati, hali inayochangia matibabu yasiyo na ufanisi na hatari kwa wagonjwa.
“Dawa duni hugharimu zaidi ya fedha, hugharimu maisha,” amesema Mchengerwa, akionya kuwa utegemezi wa uagizaji kutoka nje umechangia pia kuenea kwa dawa zisizokidhi viwango, jambo linalosababisha kushindwa kwa matibabu, usugu wa dawa na vifo vinavyoweza kuepukika.
Kuimarisha mazingira ya uwekezaji
Serikali pia imetangaza kuanzishwa kwa makundi ya vitovu vya uzalishaji wa dawa katika maeneo ya Mloganzila na Kibaha mkoani Pwani.
Vitovu hivyo vitakuwa na mifumo jumuishi itayowaunganisha wazalishaji, wasimamizi wa udhibiti, taasisi za utafiti na miundombinu ya usafirishaji, ili kupunguza gharama na kuharakisha uzalishaji.
Serikali imewahakikishia wawekezaji ulinzi wa soko mara watakapozalisha dawa zenye ubora unaokubalika kimataifa.
“Hakuna mwekezaji atakayejenga kiwanda Tanzania kisha akakandamizwa na uingizaji wa dawa zisizo na ushindani wa haki,” amesema waziri huyo.
Amesema Serikali itatumia sera, udhibiti, ununuzi wa umma na mifumo ya kodi kulinda uwekezaji wa ndani.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai, ameonesha eneo la viwanda vya dawa lililotengwa lenye ukubwa wa mita za mraba 40,000, lililopo Kibaha karibu na kituo cha SGR, kwa umbali wa kilomita 56 kutoka jiji la Dar es Salaam.
“Eneo hili limepimwa na lina huduma zote muhimu za kijamii, umeme, maji na kutakuwa na maghala pia eneo hili,” amesema.
Mavere amesema mwaka wa fedha 2024/2025, Tanzania ilipokea bidhaa za afya zenye thamani ya Sh1.2 trilioni, sawa na Dola milioni 491 za Marekani, huku asilimia 56 ikiwa ni kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Munde, amesema kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP), Serikali imeandaa mfumo wa kisheria wa PPP Act ya mwaka 2023 ili kuwezesha na kulinda fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Viwanda vya Dawa Tanzania (TPMA), Bashiru Haruna, amesema kuundwa kwa kikosi kazi cha kushughulikia masuala ya uwekezaji kumechangia kuweka mwelekeo sahihi na kujenga mazingira mazuri ya kukuza viwanda vya bidhaa za afya.
Amebainisha hatua hiyo itachochea ukuaji wa uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza utalii wa tiba (medical tourism).
Mpaka sasa, jumla ya wawekezaji 40 wamejitokeza kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa za afya nchini Tanzania, huku 25 kati yao wakihudhuria mkutano huo maalumu, wakitokea nchi za Dubai, Misri, Ujerumani, Somalia, Saudi Arabia, Sudan Kusini, Kenya, China, Rwanda, Ethiopia na India.