Sh300 milioni kuimarisha kilimo cha mwani Zanzibar

Unguja. Katika kuendeleza na kuimarisha kilimo cha mwani Zanzibar, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar wamezindua mradi wa utafiti wa zao hilo na matumizi ya teknolojia kuchochea ukuaji wake.

Mradi huo unaotarajia kutumia Sh300 milioni, mbali na Zanzibar utafanyika pia Mafia na Bagamoyo kwa Tanzania bara.

Akizungumza wakati wa kuzindia mradi huo Januari 19, 2026, Ofisa uratibu Wizara ya Uchumi wa Buluu, Omar Saleh Moh’d amesema sekta ya mwani ina mchango mkubwa wa kuinua uchumi kwa jamii hivyo hakuna budi kwa Serikali kufanya tafiti mbalimbali za kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea kuingia kwa maradhi katika zao hilo baharini.

“Miongoni mwa sekta muhimu hapa nchini ni ukulima wa mwani kutokana na zaidi ya watu 36,000 hususani wanawake na vijana wamejiajiri kupitia sekta  hiyo,” amesema.

Wanawake wakulima wa mwani, wakiendelea kufunga mwani kwenye kamba kwa ajili ya kupanda eneo la Paje Mkao wa Kusini Unguja.



Kilimo cha mwani kibiashara kilianza mwaka 1989 Visiwani Zanzibar nakuenea Tanzania bara katika miaka 1990 na zaidi ya watu 36,000 wanapata riziki zao kupitia zao la mwani.

Kwa upande wake Mtafiti Kiongozi wa mradi huo, Dk Amelia Buriyo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema tafiti mbalimbali zitaendelea kufanyika katika kilimo cha mwani ili kuondoa  changamoto za upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima na  kudhibiti maradhi yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi baharini.

“Mradi huu utaleta majibu kwa wananchi na kutafuta mikakati ya kuimarisha ili kuweza kudhibiti changamoto tunazozipitia kwenye ukulima wa  mwani ikiwa janga la asili ambalo hakuna mtu hata mmoja anaweza kulidhibiti kwa mikono yake,” amesema.

Sambamba na hilo amefafanua kuwa maeneo yatakayofanyika utafiti huo ni Unguja, Pemba, Mafia Dar es Salaam na Bagamoyo pamoja na kusomesha wanafunzi wanne ngazi ya umahiri, wawili ngazi ya uzamivu ili kuongeza wataalamu kwenye maeneo husika.

Ashura Said Haji mkulima wa mwani, amesema mradi huo umekuja kwa wakati muafaka kwani hivi sasa bahari imechafuka na kujitokeza maradhi ya yanayoathiri zao hilo.

“Tunaamini mradi huu itatusaidia sisi wakulima na kuleta tija katika kilimo cha mwani kwa sababu kuna changamoto nyingi zinazotukabili, likiwemo suala zima la mbegu, mabadiliko ya tabianchi na hata kina kifupi cha bahari,” amesema.

Jumla ya Sh300 milioni zimetengwa kwa ajili ya kuendesha mradi wa kujenga mfumo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi baharini unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia.