Bagamoyo. Ukosefu wa nyumba salama kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia umeendelea kuwa chanzo kikubwa cha maumivu ya ziada kwa wasichana wanaokumbwa na vitendo hivyo nchini.
Badala ya kupata hifadhi ya muda, usalama na huduma za kisaikolojia baada ya kupitia ukatili, wasichana wengi hulazimika kurejea katika mazingira yaleyale yaliyowadhuru, hali inayoongeza hatari ya ukatili unaojirudia na kuathiri zaidi afya zao za mwili na akili.
Kukabiliana na hilo, Shirika la Msichana Initiative limeanza ujenzi wa kituo maalumu ambacho kitakuwa nyumba salama kwa wasichana walioathirika na vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati wakiendelea kupigania haki zao.
Kituo hicho kinachojengwa Kiromo, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kitakuwa cha tano Tanzania huku bado kukiwa na uhitaji wa vituo vya aina hiyo kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika wa matukio ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza leo Januari 19, 2026 wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kituo hicho, Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti amesema harakati dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia zinakumbana na changamoto ya nyumba salama kwa waathirika, hali inayosababisha waendelee kupitia maumivu.
Amesema shirika hilo kupitia mkakati wake wa 2023-2027, ilibaini pengo hilo la ukosefu wa makazi salama ya uhakika yanayozingatia mahitaji ya mtoto wa kike ambayo yanaunganisha ulinzi, haki na uponyaji.
Amesema wasichana wanaonusurika katika ukatili, zaidi ya kuokolewa, wanahitaji matunzo, mwongozo, na muda wa kupona huku wakisaka haki.
“Tunafahamu kwamba maelfu ya wasichana nchini Tanzania wanaishi katika hofu, ukatili, ndoa za utotoni, mimba za mapema na kunyimwa haki ya elimu na afya.
“Wasichana wengi wanapokimbia ukatili, hawana mahali salama pa kwenda. Mara nyingi wanarudishwa kwenye mazingira hatarishi kwa sababu hakuna nyumba salama za kutosha,” amesema.
Consolata amebainisha kuwa baada ya kukamilika, kituo hicho kitatoa makazi ya muda kwa wasichana waliokumbwa na ukatili, msaada wa kisheria, huduma za kisaikolojia na shamba darasa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na ujuzi wa kujitegemea.
Uzinduzi wa kituo hicho umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 10 ya shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kutetea haki za wasichana, ikiwa ni pamoja kulinusuru kundi hilo na ndoa za utotoni.
Mwanzilishi wa shirika hilo, Rebeca Gyumi amesema kuanza ujenzi wa kituo hicho ilikuwa ndoto ya muda mrefu katika kuunga mkono juhudi za kuwanasua wasichana katika mazingira hatarishi yanayowasababishia kupitia ukatili.
“Katika kipindi chote tulichofanya kazi tuliiona changamoto hii, tukaona kuna haja ya kuwa na nyumba salama ambapo wasichana wanaonusurika au walioathirika na vitendo vya ukatili wapate hifadhi, wakati mchakato wa kutafuta haki ukiendelea.
“Ujenzi huu unahitaji Sh4 bilioni, wito wetu kwa wadau wengine na kila anayeguswa na haki za wasichana na wanawake achangie ili tulikamilishe hili na kituo kianze kufanya kazi kwa lengo lililokusudiwa,” amesema.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Stella Msofe amesema uwepo wa kituo hicho katika wilaya hiyo utaenda kuipunguzia mzigo Serikali hasa katika kipindi hiki ambacho matukio ya ukatili yameshika kasi.
“Bagamoyo matukio ya ukatili yapo na waathirika wapo, unaweza kukuta mtoto ametelekezwa na wazazi wake sasa kituo hiki japo kitachukua wasichana kutoka maeneo mbalimbali nchini, kitakuwa msaada mkubwa kwa wilaya yetu.
“Serikali kwa upande wetu tutatoa kila aina ya msaada kuhakikisha kinajengwa na kinaanza kutoa huduma, niwaombe wadau wengine na wote tunaoguswa katika hili tuchangie ili mawazo haya mazuri tunaona utekelezaji wake kwa manufaa ya wasichana na jamii kwa ujumla,” amesema Stella.