Dar es Salaam. Moja ya changamoto sugu zinazowakabili wakazi wa maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam ni upatikanaji wa usafiri wa daladala, hali ambayo imekuwa ikisababisha msongamano mkubwa katika vituo na kulazimu baadhi ya abiria kupandia madirishani, huku wengine wakipata majeraha kutokana na kugombea nafasi za kupanda.
Kero hiyo imechukua sura mpya katika baadhi ya maeneo ambako watu wamejiajiri kuwashikia abiria viti ndani ya daladala kwa ujira wa Sh500. Utaratibu huo unaonekana kushamiri zaidi katika daladala zinazofanya safari kati ya Gongo la Mboto na vituo vya Mbezi Luis pamoja na Kipaya, hususan katika magari yanayokwenda Chanika.
Hata hivyo, hali ni tofauti kwa abiria wanaosafiri kwenda maeneo ya Msakuzi, Msumi na Mpigi Magohe, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo, ambako upandaji wa daladala hufanyika kwa utaratibu wa kupanga foleni.
Abiria wakiwa wamepanga foleni ya kuingia kwenye daladala katika kituo cha mabasi cha Mbezi Mwisho. Picha na Ally Mlanzi
Abiria wa maeneo hayo wanasema mfumo huo umewasaidia kupunguza vurugu, kuepuka majeraha na kuondoa hatari ya kuibiwa na vibaka.
Wanasema nyakati ambazo idadi ya abiria inapokuwa ndogo, kila mmoja hupanda kwa utulivu bila msongamano wala kugombea.
Mwananchi imefika katika kituo hicho na kufanya mazungumzo na abiria wanaotumia daladala hizo kila siku, pamoja na madereva na makondakta, ili kufahamu chanzo na sababu za kuanzishwa kwa utaratibu huo wa kupanga foleni pamoja na faida zake katika kuboresha usalama wa abiria.
Akieleza chanzo cha kuanzishwa kwa utaratibu wa kupanga foleni, Msimamizi wa daladala zinazotoa huduma katika maeneo hayo, Mwishehe Sultan akizungumza na Mwananchi, amesema mfumo huo ulianza mwaka 2022 wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19, kipindi ambacho Serikali ilikuwa ikihamasisha wananchi kupanda vyombo vya usafiri kwa kufuata foleni ili kudhibiti maambukizi.
Hata hivyo, Sultan amesema licha ya maeneo mengine kuachana na utaratibu huo baada ya janga hilo kupungua, wao waliamua kuendelea nao kutokana na faida zake nyingi, ikiwemo kudhibiti vitendo vya wizi vilivyokuwa vikifanywa na vibaka wakati wa msongamano wa abiria wanaogombea kupanda daladala.
Amesema vibaka hutumia fursa ya vurugu na umati wa watu kugombea magari kuiba mali za abiria, hali ambayo imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa kupanga foleni.
Sultan amesema kila abiria humwona aliye mbele yake na hivyo kuongeza uwajibikaji na uangalizi.
“Vibaka huwa na mbinu zao wanapotaka kuiba. Wanapoona umati wa watu unagombea gari, hutumia nafasi hiyo kuiba. Utaratibu huu umeepusha mambo mengi kwa sababu mtu wa nyuma humwona wa mbele, hivyo ni rahisi kubaini kinachotokea,” amesema Sultan.
Abiria wakiwa wamepanga foleni ya kuingia kwenye daladala katika kituo cha mabasi cha Mbezi Mwisho.
Aidha, amesema upangaji wa foleni huonekana zaidi daladala zinapokuwa chache, hususan nyakati za jioni watu wanapotoka kazini na wanafunzi wanaporejea kutoka shuleni.
Hali kama hiyo pia hujitokeza siku za mwishoni mwa wiki, idadi ya abiria huongezeka kutokana na baadhi yao kwenda kuangalia mashamba, viwanja au nyumba walizoanza kujenga katika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kwa Yusufu, eneo ambalo kituo hicho kipo, Gasper Msibo ameunga mkono maelezo ya Sultan na kusema kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu huo, ofisi yake ilikuwa ikipokea malalamiko ya wizi karibu kila siku kutoka kwa abiria wa ruti hiyo.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya uongozi wa mtaa na wasimamizi wa ruti, na kuongeza kuwa utaratibu huo ungekuwa mzuri zaidi kama ruti nyingine nazo zingeuiga.
Naye Shabani Khamis, mmoja wa makondakta kwenye daladala hizo amesema mfumo wa foleni umesaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku sambamba na kulinda magari dhidi ya uharibifu unaosababishwa na msongamano wa abiria.
Amesema awali, abiria walikuwa wakiminyana mlangoni na kupandia madirishani, hali iliyosababisha kuvunjika kwa vioo na kuharibika kwa milango ya magari, jambo lililoongeza gharama za matengenezo kwa madereva na wamiliki wa daladala.
“Sisi madereva utaratibu huu umetusaidia sana, kwa sababu abiria hawaminyani tena mlangoni wala kupandia madirishani. Mara nyingi uharibifu ukitokea, mmiliki wa gari haelewi kuwa ni msongamano wa abiria uliosababisha,” amesema.
Mmoja wa abiria wa daladala hizo, Pascal Mageleja amesema mfumo wa kupanga foleni umeondoa adha ya kugombea magari na kuongeza utulivu katika vituo.
Amesema pamoja na kupunguza vitendo vya wizi, utaratibu huo umewasaidia wajawazito, watoto na wazee, ambao awali walikuwa wakikumbana na hatari ya kuumia au kushindwa kabisa kupata usafiri kutokana na kukosa nguvu ya kuyagombea.
Katika ushauri wake, Mageleja amesema utaratibu huo unaweza kuanzishwa pia katika maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam iwapo wasimamizi wa vituo husika watausimamia ipasavyo kama inavyofanyika katika eneo lao.
Naye Winis Wiston amesema utaratibu wa foleni ni mzuri kwa abiria wasio na haraka, lakini akabainisha kuwa ucheleweshaji hutokea kutokana na upungufu wa magari unaosababishwa na miundombinu duni ya barabara.
Amesema kuna nyakati abiria hulazimika kusubiri kituoni kwa zaidi ya saa moja bila kupita daladala, hivyo foleni inakuwa ndefu hali inayoongeza hatari ya kuchelewa kufika wanakokwenda.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa Serikali kuboresha barabara katika maeneo hayo, akisema hatua hiyo itawavutia wamiliki wa daladala kuongeza idadi ya magari, kuboresha upatikanaji wa usafiri na kuchangia ukuaji wa uchumi wa maeneo husika pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Madereva na Makondakta Mkoa wa Dar es Salaam (Uwamadar), Shukuru Mlawa amepongeza kuanzishwa kwa utaratibu huo na kueleza kuwa atashirikiana na wadau husika kujifunza namna ulivyoanzishwa ili uweze kufanyika katika ruti nyingine.
Hata hivyo, amesema ustaarabu wa kupanga foleni unapaswa kuanzia kwa abiria wenyewe, akisema Jiji la Dar es Salaam lina idadi kubwa ya magari na iwapo abiria watazingatia nidhamu hiyo, daladala zinaweza kuondoka kila baada ya dakika 10 badala ya kusimama kituoni kwa dakika 20 au zaidi zikisubiri abiria.
Ameongeza kuwa msaada wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, unaweza kuimarisha utekelezaji wa utaratibu huo, kama wanavyofanya katika kudhibiti magari yanayokiuka ruti au kushindwa kukaa kwenye mstari wakati wa kupakia abiria.
Naye Katibu wa Taifa wa Shirika la Kutetea Haki za Abiria (Shakua), Hashim Omar amesema mfumo wa kupanga foleni ni mzuri na unaweza kuleta matokeo chanya endapo utaanzishwa katika maeneo mengine.
amesisitiza umuhimu wa elimu kwa abiria, madereva na wamiliki wa daladala kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).
Hata hivyo, Omar ametoa tahadhari kuwa utekelezaji wake unaweza kuathiri abiria wanaopanda katika vituo vya njiani.
Amesema changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kwa makubaliano ya kupandisha abiria kwa kiwango fulani katika vituo vya mwanzo, ili kuwaacha wanaopanda njiani wapate nafasi ama kwa kupakia abiria asilimia 75 na nafasi zilizobaki kujazwa njiani.
“Hili linawezekana kabisa endapo kutakuwa na elimu kwa wadau wote kuanzia abiria, madereva hadi wamiliki wa daladala, kwa kuwa kila mmoja huwa na hesabu zake na wengine huona kukaa kwenye foleni kama kikwazo cha kupata mapato,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema utaratibu huo ni wa kupongezwa na unaostahili kuigwa.
Hata hivyo, amesema utekelezaji wake katika maeneo ya katikati ya jiji unaweza kuwa mgumu kutokana na msongamano mkubwa wa abiria, presha ya muda na hali ya baadhi ya abiria kutaka kuwahi, kiasi kwamba hata aliyekuwa wa kwanza kufika mlangoni, anaweza kuchelewa au kukosa kabisa nafasi ya kupanda.