TEMDO YABUNI MTAMBO MPYA WA KUCHAKATA MIWA KUONGEZA UZALISHAJI WA SUKARI

 


SHIRIKA la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) limebuni, kusanifu na kutengeneza mtambo wa kuchakata zao la miwa ili kupata sukari kwa kiwango cha mjasiriamali wa kati, ikiwa ni jitihada za kupunguza uhaba wa sukari nchini pamoja na kuwaongezea wakulima wa miwa soko la uhakika.

Hayo yalisemwa Januari 19, 2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb.), wakati wa Ziara yake TEMDO jijini Arusha ambapo amelishauri Shirika hilo kuzalisha mitambo hiyo ya Sukari pamoja na mitambo mingine katika kanda zote nchini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani ikiwemo TAMISEMI na nje ya nchi, ili kufikia Malengo yanayotarajiwa.

Aidha, aliiagiza TEMDO kuzalisha mitambo inayoendana na kasi ya teknolojia ili kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa zinaingia sokoni na kutoa fursa zaidi za kiuchumi na kuondokana na umaskini kwa Wajasiliamali na Wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TEMDO, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, alisema Shirika hilo linaendelea kuweka mikakati madhubuti ya mageuzi ya viwanda kwa kuzalisha mitambo itakayotatua changamoto za wakulima na kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ili kuongeza uzalishaji viwandani na kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, Profesa Frederick Kahimba alisema
kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza pengo la uzalishaji wa sukari nchini sambamba na kuongeza thamani ya zao la miwa kwa wakulima wadogo na wa kati ambapo hadi sasa Shirika hilo limepokea maombi sita kutoka kwa Wajasiliamali wa kati wanaotaka kufungiwa mitambo hiyo ya Sukari kutoka Dodoma, Same, Manyara, Busega, Kilosa na Morogoro.

Temdo inazalisha bidhaa zaidi ya 16 ikiwemo vifaa tiba vya hospitali kama majokofu ya kuhifadhia maiti, vichomea taka hatarishi, vitanda vya aina mbalimbali vinavyohitaji kufika soko la Zanzibar ili kuongeza pato la Taifa, kukuza uchumi na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi. Alifafanua Kahimba.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango wa wizara hiyo, Audax Bahweitama akimwalikilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema Serikali improvises Sera na Sheria mbalimbali zinazohusu Maendeleo ya Viwanda ili kufikia uchumi jumuishi kupitia viwanda kwa kuzalisha bidhaa zenye ushindani na ubora sokoni, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.