Wanachama 27 wajitokeza kumrithi Jenista, vikao kuamua

Songea. Wanachama 27 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Vijijini wamejitokeza kuchukua fomu za kutia nia kugombea ubunge Jimbo la Peramiho ili kujaza nafasi iliyoachwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jenista Mhagama.

Jenista alifariki dunia Desemba 11, 2025 jijini Dodoma kutokana na maradhi ya moyo na Desemba 16, 2026 alizikwa katika Kijiji cha Luanda kilichopo katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kufungwa shughuli ya uchukuaji fomu ambayo ilianza  Januari 18, 2026 na kufungwa Januari 19, 2026 saa 10:00 jioni, Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Juma Nambaila amesema wanachama 28 walichukua fomu ambapo kati yao wanaume ni 21 na wanawake ni sita.

Nambaila amesema   27 wamefanikiwa kurejesha fomu zao lakini mmoja ameshindwa kufanya hivyo. Katibu huyo amekataa kubainisha jina la mwanachama huyo akidai kwamba wote ni wanachama wa CCM.

Amesema watiania hao wote watapigiwa kura Januari 21, 2026 kwenye kata zao na hakutakuwa na vikao vya kuwatambulisha kwenye kata kama ilivyokuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amefafanua kuwa uchaguzi huo ni wa kipekee, hakuna mwanachama atakayekatwa jina bali majina yote yatapigiwa kura na wajumbe na kisha vikao vya uamuzi na kikanuni vitakaa na kupitia majina yote na kupendekeza na kisha kuyapeleka ngazi ya mkoa na Taifa.

“Uchaguzi huu ni wa kipekee, ni tofauti na wa 2025, baada ya kuchukua fomu tulikuwa na vikao vya mapendekezo ambapo watia nia walikatwa na kubakiza majina matatu ambayo yalipigiwa kura. Hii ni tofauti, wote watapigiwa kura na baada ya hapo vikao vya kikanuni vitakaa kupitisha jina la mgombea,” amesema Nambaila.

Amewashukuru waandishi wa habari kwa kujitoa kwao na vyombo vyao kutangaza uchaguzi huo, hali ambayo imesaidia kuhamasisha wanachama wengi kujitokeza kugombea licha ya muda kuwa mfupi.

Pia, amewashukuru wagombea wote waliojitokeza kuchukua na kurejesha fomu zao.