Wanaodaiwa kutakatisha Sh346 milioni za CRDB, NBC wamwangukia DPP

Dar es Salaam. Raia wa Bulgaria, Eduardl Mladenov (32) na Mtanzania Juma Ndambile (58) wanaodaiwa kujihusisha na miamala ya kutoa fedha katika Benki za CRDB na NBC, wamemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wakiomba kufanya majadiliano ya kukiri makosa (plea bargaining) ili kuimaliza kesi inayowakabili.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita, yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa na kujihusisha na miamala ya kutoa fedha yenye thamani ya Sh364 milioni kutoka Benki za CRDB na NBC.

Pia wanadaiwa kukutwa na mali ya wizi, ikiwamo mashine ya kuchanja kadi kwa ajili ya kufanya malipo ya kielektroniki (POS), yenye thamani ya Sh500,000 mali ya Selcom Tanzania.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Januari 19, 2026 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Kupitia wakili wao, Steven Luko, washtakiwa wamedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo kuwa tayari wameandika barua kwa DPP kuomba majadiliano ya kukiri makosa, lakini hadi sasa hawajapata majibu.

Akijibu, wakili wa Serikali, Roida Mwakamele ameeleza kuwa barua hiyo bado inafanyiwa kazi na kuomba upande wa utetezi uvumilie.

Kuhusu upelelezi, amedai bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Swallo amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2026 kwa ajili ya kutajwa. Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba 12, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 29134 ya mwaka 2025, yenye mashtaka sita.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa. Inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2025 hadi Novemba 11, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge hilo.

Shtaka la pili ni kupatikana na mali ya wizi, linalomkabili Ndambile pekee, inadaiwa Oktoba 24, 2025 katika eneo la Mbweni, Wilaya ya Kinondoni alikutwa na mashine ya POS yenye thamani ya Sh500,000, mali ya Selcom Tanzania.

Shtaka la tatu ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Julai Mosi, 2024 hadi Novemba 11, 2025, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walijipatia Sh116 milioni kutoka Benki ya NBC.

Shtaka la nne nalo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo katika kipindi hichohicho walijipatia Sh248 milioni kutoka Benki ya CRDB PLC.

Shtaka la tano na la sita ni ya utakatishaji fedha yanayowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kuwa walijihusisha na miamala ya moja kwa moja ya fedha taslimu za Kitanzania Sh116 milioni kutoka NBC na Sh248 milioni kutoka CRDB PLC, huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.