Winga Mzenji, Fountain Gate kuna kitu

UONGOZI wa Fountain Gate uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa JKU FC ya visiwani Zanzibar, Tariq Mohamed Mkonga, baada ya pande mbili kati ya nyota huyo na mabosi wa kikosi hicho kufikia hatua nzuri.

Chanzo kutoka katika kikosi hicho, kililiambia Mwanaspoti mazungumzo kati ya upande wa mchezaji na uongozi wa Fountain Gate yamekamilika, ambapo tayari nyota huyo amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza.

“Makubaliano ya awali ni ya mkataba wa miaka miwili yenye kipengele cha kuongeza mwingine mmoja ikiwa benchi la ufundi litaridhika na kiwango chake, tunaendelea na maboresho ya nafasi mbalimbali zilizopendekezwa,” kilisema chanzo hicho.

Mkonga mwenye uwezo mkubwa wa kucheza winga zote mbili ya kushoto na kulia, huku akitokea pia nyuma ya mshambuliaji, anaungana tena na nyota mwenzake aliyecheza naye JKU, kiungo, Saleh Masoud Abdallah ‘Tumbo’, aliyeachana na Pamba Jiji.

Nyota huyo aliyejiunga na Pamba msimu wa 2024-2025, akitokea Klabu ya JKU ya kwao visiwani Zanzibar, aliomba uongozi wa kikosi hicho kuvunja mkataba wake uliobakia ili akatafute changamoto mpya na ndipo mabosi wa Fountain Gate wakamsajili.

Mbali na Mkonga na Saleh, nyota mwingine aliyejiunga na kikosi hicho ni mshambuliaji, Boniface Mwanjonde aliyeachana na Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, ambayo msimu huu ameifungia mabao tisa katika mechi 14 alizocheza.