Chawata mtaa kwa mtaa kuwasaka wenye ulemavu, ikilia ukata

Mbeya. Wakati idadi ya watu wenye ulemavu wa viungo wakifikia 1,370 mkoani Mbeya, Chama cha wenye ulemavu huo mkoani humo (Chawata), kimesema kinatarajia kufanya ziara ya mtaa kwa mtaa kuwabaini wenye ulemavu wakiwamo watoto, kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.

Hata hivyo, kimeeleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni nguvu ya kifedha kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kutokana na kutokuwa na chanzo rasmi cha mapato kurahisisha utendaji kazi.

Akizungumza leo Januari 20, Mwenyekiti wa Chama hicho, Evance Mwakyusa amesema kwa mwaka 2025, jumla ya wenye ulemavu wa viungo walikuwa 1,370 huku Kyela ikiwa kinara wa kundi hilo.

Amesema pamoja na idadi hiyo, wanaume ndio wanaongoza (bila kutaja idadi), akieleza kuwa bado takwimu za watoto wenye ulemavu ziko chini kulingana na taarifa za jamii na familia husika.

“Hizi takwimu ni kwa wale tulionao kwenye kanzidata, hivyo hii ziara tunayotarajia kufanya mapema mwezi Februali itabaini wengine ambao hawajaripotiwa ili kuisaidia hata serikali kujua namna ya kutusaidia.

“Idadi kubwa katika kundi hili wengi ni wanaume, kwa sababu kuna wanaozaliwa wakatambuliwa mapema, lakini inakuja kuongezeka kupitia vyombo vya moto ikiwa ni pikipiki yaani bodaboda na bajaji,” amesema Mwakyusa.

Amesema kuwa chama hicho kinakabiliwa na changamoto ya kifedha kuwawezesha kuwafikia wengine wenye uhitaji ikiwamo elimu, akiomba wadau kuwasaidia ili kufikia malengo na kuwakwamua.

Mmoja wa wenye ulemavu wa viungo, Festo Mwanjala amesema kundi hilo limeachwa nyuma kwakuwa hata huduma za msingi ikiwamo kujumuishwa na wengine akiomba kuwapo mazingira rafiki kwao.

Hata hivyo amepongeza baadhi ya viongozi wa watendaji wa serikali kulitambua kundi hilo na kuliingiza kwenye mikopo ya asilimia 10, akiomba serikali kuongeza asilimia haswa upande wa kundi hilo.

“Kwakuwa wengi tuna changamoto ya viungo, watuongezee asilimia ili tuweze kubadilika kiuchumi na kuondokana na utegemezi, tupo baadhi tunaojituma katika utafutaji na wengine wanategemea misaada,” amesema Mwanjala.