DIWANI MAPUNG’O AWABANA WASIMAMIZI WA MIRADI JIMBO LA MUSUKUMA

Diwani wa kata ya Butobela Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Pascal Mapung’o amewataka wasimamizi wa miradi ya maendeleo jimboni Geita kuzingatia maelekezo ya utekelezaji wa miradi yanayotolewa na Halmashauri.

Mhe Mapung’o ameyasema hayo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyofanyika Januari 19,2026 katika jimbo la Geita ambalo Mbunge wake ni Mhe Joseph Musukuma.

Aidha katika ziara hiyo Mhe Pascal Mapung’o amewataka Wahandisi wa Halmashauri kuhakikisha wanashughulikia kasoro zote ambazo zimeonekana kwenye miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutumika.

“Kasoro zote ambazo tumeziona kwenye miradi zifanyiwe kazi kwa wakati ili miradi ikamilike kwa wakati na kuanza kutumika” Amesema Mhe Mapung’o

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji Bi Sarah Yohana ambaye pia ni Afisa Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Geita amewataka mafundi ujenzi wanaotekeleza miradi hiyo kuongeza kasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

“Niwatake mafundi kuongeza kasi ya ujenzi ikiwa ni pamoja na wasimamizi wa miradi hii kuwalipa mafundi ujenzi kwa wakati” Amesema Bi Sarah

Vilevile Bi Sarah ametoa wito kwa Wasimamizi wa miradi kuwashirikisha wananchi katika maeneo yao utekelezaji wa miradi na kuwajulisha wananchi fedha za miradi zinapoingia ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu miradi ya maendeleo.

Kamati hiyo ikiwa na wataalam kutoka Halmashauri, imetembelea miradi ya ujenzi wa shule, ukarabati wa miundombinu ya madarasa,ujenzi wa nyumba za watumishi Pamoja na uzio katika nyumba hizo miradi ambayo thamani yake ni kiasi cha Shilingi Bilioni 2.1. fedha hizo zikiwa ni ni Mapato ya ndani, BOOST na wajibu wa Kampuni ya mgodi wa dhahabu wa Geita kwa jamii (CSR-GGML)

Ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa jamii.