Dk Migiro awatumia ujumbe mawaziri, wabunge

Dodoma/Singida. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro amewataka viongozi wa ngazi za juu wakiwamo wabunge na mawaziri kuhudhuria vikao vinavyoitishwa na mabalozi wa mashina yao kujua changamoto zinazokikabili chama, jamii na Taifa kwa jumla ili kuzitatua.

‎‎Dk Migiro ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 20, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na mabalozi wa mashina wa Mkoa wa Dodoma.

‎Amesema ngazi ya shina ndiyo iliyo karibu na wananchi na wanajua changamoto zote zinazowakabili wananchi,  hivyo ni muhimu kuhudhuria vikao na mikutano inayoitishwa na mabalozi wa mashina ili kuzijua na kuzitatua.

Mabalozi wa mashina wa Mkoa wa Dodoma wakiwa katika mkutano wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro.



‎Amesema hiyo itasaidia kujua changamoto hasa za vijana walioko kwenye mfumo rasmi wa ajira na wale ambao hawapo kwenye ajira ili kujua ni namna gani wanaweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto hiyo ya kukosa ajira.

‎”Naomba kutoa wito kwa wale viongozi wote ambao bado hawawajibiki kushiriki kwenye vikao vinavyoitishwa na mashina, na hapa nipende kuwatambua viongozi wa ngazi zote kama wabunge na mawaziri,kuwepo kwenu hapa kunaonesha ni namna gani mna mchango mkubwa.

“Nawaomba viongozi wa mkoa na hili mkalizungumze kila mahali kwamba, viongozi washiriki kule chini kwenye miradi ya chini,” amesema Dk Migiro

‎“Hata kwangu mimi ninapoishi huwa nahudhuria kwenye vikao vinavyoitishwa kwenye shina langu, tumeona kwa viongozi wa kitaifa wakipita na kusikiliza kero za wananchi na sisi sasa tushiriki kwenye vikao vya mashina kwa sababu ndiyo vipo karibu sana na wananchi.”

‎Mbali na hilo, amewataka mabalozi wa mashina kufanya vikao vya Kikatiba kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi ili vikao hivyo viweze kuibua fikra chanya kwa maendeleo ya wananchi wenyewe.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro akizungumza leo Jumanne Januari 20, 2026 katika mkutano wa mashina wa Mkoa wa Dodoma.



‎Aidha, amewataka mabalozi wa mashina kutambua shughuli zote za kiuchumi  zinazofanywa na vijana kwenye maeneo yao ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili.

‎Dk Migiro amewapongeza mabalozi hao kwa ushindi wa kishindo wa CCM kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 na kwamba wao ndiyo ngazi ya mafanikio ya ushindi wa chama hicho.

‎Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amewataka viongozi wa taasisi na dini kufanya shughuli zao na kuacha kukifuatilia chama hicho kwa kuwa, kwa kufanya hivyo hawatakubali, vinginevyo wabadilishe kazi na kujiunga na chama hicho.

‎Amesema kumekuwepo na ushauri, maoni na lugha za matusi kuhusu CCM jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa chama hicho ni kikubwa, hivyo wanaofanya hivyo waache mara moja.

‎“Kuna wengine wanataka kupata umaarufu kupitia CCM kwa kuitukana na kuikejeli, hilo halikubaliki. Siyo kwamba hatupendi maoni na ushauri, lakini iwe kwa nia njema ya kujenga na siyo matusi na kejeli,” amesema Kimbisa.

Mabalozi wa mashina wa Mkoa wa Dodoma wakiwa katika mkutano wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro.



‎Kwa upande wao mabalozi wa mashina wameomba kupatiwa bima ya afya kwa ajili ya matibabu na kupatiwa mikopo ya halmashauri ili waweze kujimudu kiuchumi.

‎Aidha, wameshukuru chama hicho kwa kuwapatia baiskeli kwa ajili ya usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine hali iliyowarahisishia kazi zao za kila siku.

‎Akisoma maoni kwa niaba ya mabalozi hao, Paulina John kutoka Wilaya ya Chamwino amesema wanahitaji bima ya afya kwa ajili ya kupata matibabu pindi wanapopata maradhi.

‎ Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM, Kenani Kihongosi ameendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho huku akipokea kero 61 za migogoro ya ardhi na maji zilizowasilishwa kwenye mikutano ya hadhara.

Miongoni mwa waliowasilisha kero hizo, yumo kikongwe Francisca Juma (93) aliyedai kufukuzwa katika nyumba aliyojenga na marehemu mumewe mwaka 1968 lakini anaambiwa ni mvamizi.

Kero hizo ziliibuliwa jioni ya Januari 19, 2026 kwenye mkutano wa kiongozi huyo uliofanyika stendi ya zamani Manispaa ya Singida.

Kihongosi katika ziara mkoani Singida amekuwa na mtindo wa kupokea kero na kuwataka wataalamu kuzitolea majibu yatakayopunguza maumivu.

Katika ziara hiyo, kero na malalamiko yaliyoibuliwa yalipatiwa majibu ya moja kwa kutoka kwa wataalamu jambo lililoibua kelele kwamba, siku zote wamekuwa wakizungushwa hata kukosa nafasi za kuwaona viongozi.

Akiwa kwenye mkutano, watu walijitokeza kuwasilisha kero na malalamiko wakieleza jinsi wanavyohangaika kupata haki zao katika ofisi nyingi.

Malalamiko ya wananchi yalionekana kumkera Kihongosi aliyelazimika kusimama kwa saa 2.17 jukwaani, akitaka kila mmoja apewe nafasi ya kuwasilisha kero yake.

“Ndugu wataalamu na viongozi lazima tusikilize kero za watu na tuzipatie ufumbuzi, yapo tunayoweza kuyatolea majibu ya papo hapo, lakini mengine yabebeni na mnipe majibu yake kabla sijamaliza ziara yangu mkoani hapa,” ameagiza Kihongosi.

Akiwasilisha malalamiko mbele ya Kihongosi, Francisca Juma amesema amekuwa akihangaika maeneo tofauti kutafuta haki ili abaki kwenye nyumba yake na kuepuka vitisho, lakini hajapata msaada.

“Tulijenga nyumba hii na marehemu mume wangu mwaka 1968, tukajenga nyingine mwaka 1970 na ilipofika 1976 mume wangu akafariki, lakini hivi karibuni kimeibuka kikundi cha vijana wananifukuza pale na kunitishia kwamba nisipotoka watanisukumia ukuta niishie ndani,” amesema Francisca.

Amesema taarifa zilishatolewa kwa viongozi na vyombo vya ulinzi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Juma Malumbe ametaja kero ya ardhi katika Kata ya Unyambwani akisema kuna upimaji unaofanyika bila kuweka uwazi na gharama za upimaji zimekuwa kubwa, hali inayofanya migogoro idumu.

Malumbe pia, ameibua suala la watoto wa kike kujiuza akisema linaanza kuota mizizi na kuharibu utamaduni wa wenyeji, lakini vyombo husika viko kimya.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe ameagizwa kuchukua kero ambazo hazikuwa na majibu ya moja kwa moja na ahakikishe anafikisha taarifa ofisini ya mwenezi mapema iwezekanavyo.

“Mkuu wa wilaya hakikisha kwanza hawa waliotoa maoni yao wasisumbuliwe, nataka wawe huru na matatizo yao yatatuliwe kwa haki,” ameagiza Kihongosi.

Hata hivyo, wananchi walimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dengedo kwamba amekuwa sehemu ya faraja kwao.

Kwa upande wake, Dengedo ameahidi kusimamia kero zote ambazo hazijatolewa majawabu ili kila mtu apate haki yake.