EACOP YAVUKA ASILIMIA 79, WANANCHI WANUFAIKA AJIRA, MIUNDOMBINU NA MAPATO

 Na Avila Kakingo, Michuzi Tv

MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unaendelea kubadilisha taswira ya uchumi na maisha ya wananchi katika mikoa inayopitiwa na mradi huo, huku ajira, miundombinu na mapato ya Serikali vikiongezeka kwa kasi kadri utekelezaji unavyokaribia ukingoni.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, mradi huo umefikia asilimia 79 ya utekelezaji hadi kufikia Desemba 31, 2025 na unatarajiwa kukamilika Julai 2026.

Hayo ameyasema leo Januari 20, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika bandari ya Dar es Salaam, amesema mbali na umuhimu wake wa kimkakati kwa sekta ya nishati, EACOP umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa Watanzania.

Msigwa amesema kuwa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2021, Watanzania wamekuwa wanufaika wakuu wa ajira zinazotokana na shughuli za ujenzi wa bomba, vituo vya kusukuma mafuta, matenki, jeti na miundombinu mingine.

“Hadi kufikia Juni 2025, jumla ya ajira 9,194 zilikuwa zimetolewa kwa Watanzania, sawa na asilimia 80 ya lengo la ajira 10,000, ambapo vijana wenye ujuzi wa chini, wa kati na wa juu wamepata fursa za kujipatia kipato na kuongeza maarifa ya kazi.” Amesema Msigwa

Ameeleza kuwa mradi huo haukuishia tu kutoa ajira, bali pia umewekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia mafunzo ya ufundi na kitaalamu.

“Vijana wengi wamepata mafunzo kupitia vyuo vya VETA na baadhi yao tayari wameajiriwa, huku wengine wakiandaliwa kuwa waendeshaji wa mradi mara baada ya ujenzi kukamilika.”

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Msigwa, itaifanya Tanzania kuwa na wataalamu wa ndani watakaosimamia uendeshaji wa mradi kwa miaka ijayo.

Kwa upande wa uchumi wa ndani, Msigwa amesema mradi wa EACOP umeongeza mzunguko wa fedha nchini baada ya kununua bidhaa na huduma zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.325 kutoka kwa zaidi ya makampuni 200 ya Kitanzania.

Amesema hatua hiyo imeimarisha biashara za ndani, kuongeza mapato ya wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanayopitiwa na mradi.

Serikali pia imeanza kuvuna matunda ya mradi huo kupitia mapato ya kodi, tozo na malipo mbalimbali, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 50 tayari zimekusanywa.

Msigwa amesema kuwa baada ya mradi kukamilika na kuanza kusafirisha mafuta, Serikali inatarajia kupata mapato ya moja kwa moja yanayokadiriwa kufikia Shilingi trilioni 2.3 kwa kipindi cha miaka 25, jambo litakaloongeza uwezo wa Serikali kugharamia huduma za kijamii na miradi ya maendeleo.

Katika upande wa miundombinu, wananchi wameendelea kunufaika na uboreshaji wa barabara zenye urefu wa kilomita 304 pamoja na ujenzi wa mitandao ya mabomba ya maji safi yenye zaidi ya kilomita 30 katika maeneo mbalimbali ya mradi.

Msigwa amesema barabara hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika shughuli za uzalishaji mali, huku upatikanaji wa maji safi ukiboresha afya na ustawi wa jamii.

Ameongeza kuwa ujenzi wa gati na miundombinu ya kupakilia mafuta katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga uko katika hatua za mwisho, hali itakayoongeza shughuli za bandari, ajira na mapato pindi mafuta yatakapoanza kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa.

Msigwa amesema mradi wa EACOP umeonesha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inaweza kuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi endapo itasimamiwa vizuri.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuleta tija endelevu kwa Taifa na vizazi vijavyo.