Edo wa Simba kuibukia Stand United

NYOTA wa zamani wa Simba, Edward ‘Edo’ Christopher yupo hatua ya mwisho kabla ya kurejea tena uwanjani baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akihusishwa na Stand United maarufu ‘Chama la Wana’, inayoshiriki Ligi ya Championship.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea pia timu za Kagera Sugar, Ruvu Shooting na Coastal Union, alikuwa anazicheza timu za mtaani kwa muda mrefu na mabosi wa Stand United wanafanya mazungumzo naye kwa ajili ya kujiunga nao dirisha hili.

Mwanaspoti linatambua hatima ya nyota huyo itaamuliwa na benchi la ufundi kabla ya dirisha la usajili halijafungwa rasmi Januari 30, 2026, ambalo lilimtumia kwa ajili ya majaribio katika mechi ya kirafiki ya timu hiyo dhidi ya Pamba Jiji.

“Kazi tumewaachia benchi la ufundi chini ya Kocha, Feisal Hau kuamua kama wataridhika naye ndio maana walitumia mechi na Pamba kumuangalia kwa sababu amekaa nje kwa muda mrefu, baada ya hapo tutafanya uamuzi wa hilo,” kilisema chanzo hicho.

Stand United ‘Chama la Wana’, ilishuka daraja msimu wa 2018-2019, ikimaliza nafasi ya 19 na pointi 44, baada ya kikosi hicho chenye maskani yake Shinyanga, kushinda mechi 12, sare minane na kupoteza 18, kikifunga mabao 38 na kuruhusu 50.

Msimu uliopita, Stand ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu na pointi 61, ambapo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.

Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Off’ nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2 na kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.

Msimu huu timu hiyo inashika nafasi ya 11 na pointi 14, baada ya kushinda mechi tano, ikitoka sare miwili na kupoteza minane kati ya 15 na kikosi hicho chenye maskani yake katika mji wa Shinyanga kimefunga mabao 19 na kuruhusu 14.