Fahamu namna ya kutofautisha video halisi na iliyotengenezwa na AI

Dar es Salaam. Ukiingia kwenye mtandao wa Instagram, X, Facebook au TikTok ni rahisi kuona mtu anatolea maoni video iliyotengenezwa na akili unde (AI) bila ya kufahamu kuwa video hiyo si halisi.

Hali hiyo inatokana na ubora wa video zinazotengenezwa na teknolojia hiyo kupitia zana kama OpenAI Sora, Runway (Gen-3 Alpha), Luma Dream Machine, Google Veo 3.1, Adobe Firefly, Hailuo Minimax na Vidu Q2.

Baadhi ya watu wameshindwa kutofautisha video halisi na zile za AI kutokana na uelewa wakati kampuni za teknolojia zikiendelea kuwekeza mabilioni ya pesa kuboresha AI, huku vita kati ya ukweli na uongo wa kidijitali ndiyo kwanza imeanza.

Wataalamu wa teknolojia wameonya, kutokana na ubora wa video hizo kuongezeka, ni rahisi kwa mtumiaji wa kawaida wa mitandao ya kijamii kuingizwa mkenge na kuamini ni tukio la kweli.

Jinsi ya kutambua video iliyotengenezwa kwanza lazima ufahamu AI bado ina makosa madogomadogo ambayo yanaweza kuwa kama ‘red flag’ katika kuitathimini.

Wataalamu katika eneo hili wanasema kuna viashiria vya kuvizingatia unapoona video mojawapo ni ubora uhafifu wa picha. Ukiona video ina ukungu, haina mwonekano angavu, au ina chenga chenga, basi unapaswa kutilia shaka uhalali wake.

Pia unaweza kutambua video isiyo halisi kupitia makosa yanayoweza kuonekana, kama vile vitu kupita katikati ya kuta au binadamu kuonekana kama katuni kwenye baadhi ya video.


Pia, macho na kupepesa kwani moja ya changamoto kubwa inayozikabili kanuni za AI kwa sasa ni kuiga tabia asilia ya binadamu ya kupepesa macho. Wataalamu wanasema video nyingi za AI zinaonyesha watu ambao hawapepesi macho kabisa, au wanakupepesa kwa namna isiyo ya kawaida (kasi sana au taratibu mno). Angalia kama macho yana mng’ao usio wa asili au kama yanaonekana kuwa na ukungu.

Aidha, mwendo wa midomo na sauti, katika video za AI, mara nyingi maneno yanayotamkwa hayawiani (sync) kikamilifu na mwendo wa midomo. Ni kama kutazama movie iliyotafsiriwa lugha. Ukichunguza kwa umakini, utaona kuna sekunde kadhaa ambapo mdomo unachelewa au unatangulia kabla ya sauti kusikika.

Vilevile, angalia maumbile kama vidole na masikio mara nyingi AI bado inapata shida sana kutengeneza viungo vya binadamu kwa usahihi, hasa vidole vya mikono na masikio.

Ukiona video ambapo mtu ana vidole sita, au  vinaonekana kuungana kama vimeyeyuka, hiyo ni ishara tosha ya AI. Vilevile, angalia kama cheni au hereni zinatokea na kupotea zinapogusana na ngozi.

Kwa upande wa mwanga na vivuli binadamu wa asili anapocheza kwenye video, vivuli hufuata mwendo wake kulingana na chanzo cha mwanga. Katika video za AI, mara nyingi vivuli huwa havieleweki au vinakaa sehemu zisizo na uhalisia.

Pia, ngozi ya mtu kwenye video ya AI inaweza kuonekana laini sana kiasi cha kupoteza vitundu vya asili vya jasho au makovu madogo ya ngozi.

Kwenye mazingira ya nyuma (Background), zana mifumo mingi ya AI hutilia mkazo sura ya mtu na kusahau mazingira ya nyuma. Chunguza kama miti, majengo, au watu wanaopita nyuma ya mzungumzaji wanaonekana kuwa na ukungu (blur) usio wa kawaida, au kama mistari ya majengo inajipinda mtu anapopita mbele yake.

Hata hivyo, zipo baadhi ya zana za AI zinazoweza kutengeneza video zisizo na kasoro kama hizo zilizochanganuliwa hapo juu. Zana kama Sora na Veo zinaweza kutengeneza video zenye uhalisia.

Zana hizo zinaweza kutengeneza video zenye uhalisia wa mwanga na kivuli, muundo wa ngozi.  Video za Veo, kwa mfano, zina uwezo wa kuonyesha vinyweleo na jasho kidogo kwenye ngozi, Miondoko ya kamera: AI sasa inaiga miondoko ya kamera ya binadamu (cinematography), ikiwemo kutikisika kidogo, jambo linalofanya video ionekane imerekodiwa na mtu aliyeshika simu.

Namna rahisi ya kuzitambua tazama macho yanavyopepesa, chunguza “Physics” ya ajabu: AI mara nyingi hukosea kwenye mambo ya asili. Kwa mfano, unaweza kuona mtu anatembea lakini miguu yake inapishana kwa namna isiyo ya kawaida, au kitu kinapotea ghafla katikati ya video.

Hany Farid, Profesa wa Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, anakazia akisema AI bado inafanya makosa kama vile ngozi ya binadamu kuonekana nyororo kupita kiasi, au kwenye hiyo video unaona mienendo ya nywele na nguo inayobadilika-badilika kwa namna isiyo ya asili.

Mbali na ubora, muda wa video pia ni kigezo kingine. Profesa Farid anasema video nyingi za AI ni fupi mno, mara nyingi hazizidi sekunde 6 hadi 10. Hii ni kwa sababu gharama ya kutengeneza video hizi ni kubwa, na kadiri video inavyokuwa ndefu, ndivyo AI inavyoelekea kufanya makosa mengi zaidi.

Mtaalamu wa elimu ya kidijitali, Mike Caulfield, anashauri sasa ni wakati wa kubadili namna tunavyoamini vitu mtandaoni. Kwamba inabidi tuanze kuziangalia video kama tunavyoangalia maandishi. Huwezi kuamini kila unachosoma kwa sababu tu kimeandikwa. Lazima uchunguze chanzo chake.

Wataalamu wanashauri kuwa jambo la muhimu hivi sasa si kuangalia tu video inavyoonekana, bali kuchunguza: Nani ameposti video hiyo? Imetoka wapi? Mazingira ya video hiyo yanashabihiana na ukweli? Je, vyombo vya habari vinavyoaminika vimethibitisha tukio hilo?