Kibabage awashtua mastaa Simba | Mwanaspoti

SIMBA imeshamtambulisha beki wa kushoto mpya, Nickson Kibabage akitokea Singida Black Stars, lakini usajili huo umewaibua mastaa wa zamani wa klabu hiyo kuukosoa na kuuona haujaongeza kitu chochote badala yake wanaona ni kufifisha ushindani.

Kibabage aliyewahi kuzitumikia KMC na Yanga, alitangazwa rasmi na Singida BS ametolewa bila malipo kwenda Msimbazi, ikielezwa ameenda kuongeza nguvu eneo la kushoto la timu hiyo lenye Anthony Mligo aliyesajiliwa msimu huu kutoka Namungo.

Hata hivyo, jambo la kushangaza ni baadhi ya mastaa wa zamani wa Msimbazi, wameonyesha kushtushwa na usajili huo wa dirisha dogo na kuwashauri viongozi wasajili wachezaji wenye uwezo na viwango vya juu.

Staa wa zamani wa klabu hiyo, Zamoyoni Mogella haamini kama Kibabage ni chaguo la kocha mpya, Steve Barker kwani haoni kama ni muda sahihi wa mchezaji huyo kujiunga na Wanamsimbazi angalau ingekuwa usajili wa dirisha kubwa.

KIBA 01


“Dirisha dogo lipo kwa ajili ya kupata wachezaji wenye uwezo mkubwa ili kuongeza nguvu katika maeneo yalionekana yana udhaifu, mfano Kibabage hakuwa katika kiwango hicho cha kuisaidia Simba katika michuano mbalimbali,” amesema Mogella na kuongeza;

“Naona wamekurupuka kusajili kama walivyofanya kwa Anthony Mligo, Yanga inazidi kuongeza wachezaji wa maana kama Allan Okello kutoka Vipers wao wanapewa mchezaji bure, ni wakati wao kujitathimini na kuheshimu hisia za maumivu za mashabiki wao.

“Miaka ya zamani tulikuwa tunacheza mpira wa miguu wa ridhaa, tofauti na sasa naamini Simba ina kamati ya usajili ambayo inafanya skauti ya wachezaji kama ipo basi isikilizwe, vinginevyo wachezaji wanaowaleta wanakuwa wanafifisha ushindani pia viongozi wawe kitu kimoja.”

KIBA 02


Mogella aliyewahi pia kuichezea Yanga, amesema ilipofikia Simba lazima iwe na mfumo vinginevyo watafanya kazi ya kutengeneza kikosi kila msimu na itakuwa fimbo ya kuwachapia wenyewe.

Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garincha’ amesema  “Kocha anayehitaji ushindani hawezi kumchukua mchezaji wa kiwango hicho, siamini kama ni mapendekezo ya kocha, hana ubavu kwa mechi ngumu, wana michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayohitaji wachezaji wenye kiwango cha juu, kwa namna hiyo hata wakimchukua mchezaji wa Ulaya hakuna atakachoweza kukifanya.”

KIBA 03


Hata hivyo, licha ya ukosoaji huyo, rekodi zinaonyesha Kibabage ni mmoja wa mabeki wazoefu wa kimataifa wa Tanzania akiwahi kung’ara na Yanga misimu miwili iliyopita, lakini amewahi kucheza soka la kulipwa Morocco na kuwa mzoefu tofauti na Mligo anayechipukia kwa sasa.