Kilichoikwamisha Savio 2025 hiki hapa

WAKATI timu zikiwa bado zinajitathmini na kujipanga upya namna zikavyoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) 2026, nyota wa Savio, Oscar Anthony ametaja sababu mbili zilizowakwamisha msimu uliopita.

Anthony anayecheza nafasi ya namba 2 (Shooting Guard) aliliambia Mwanaspoti kutokuwa na maandalizi mazuri kulichangia kupoteza michezo yao ya mwanzo.

“Kwa kweli sababu hiyo ilifanya hata idadi ya wachezaji waliokuwa wanaudhuria katika mchezo kuwa ndogo na kumpa kocha wakati mgumu wa kubadilisha mchezaji,” alisema Anthony na kuongeza, pia kuchelewa kuwasili kwa wachezaji wa kimataifa kuliwafanya kuchaza kwa tahadhari kubwa.

Hata hivyo, alisema licha ya wachezaji hao kucheza michezo saba ya mwisho, Ntibonela Bukeng raia wa Uganda aliibuka mfungaji bora wa ligi hiyo mwaka jana kwa kufunga pointi 372 akimwacha kwa mbali mchezaji mwenzake Godfrey Swai aliyefunga pointi 277.

”Kwa kweli endapo wachezaji hao wote wangekuwepo mapema, naamini tungefika hata fainali bila ya kikwazo chochote,” alisema Anthony na kuongeza mwaka huu 2026 wamejipanga kurudisha heshima ya timu hiyo iliyopotea miaka sita iliyopita.

“Kwa kweli tumejipanga vizuri, ndiyo maana tumeanza maandalizi mapema na kila mchezaji anafanya mazoezi katika viwanja tofauti,” alisema Anthony.

Alisema kwa upande wake amekuwa akifanya mazoezi binafsi kwenye Uwanja wa Donbosco, Upanga na wakati mwingine anafanya pamoja na timu ya Magone ambayo ni timu ya pili ya Savio.

Alisema tangu mwaka 2024, ligi hiyo imekuwa na mabadiliko makubwa kutokana na baadhi ya timu kupata wafadhili uliowawezesha kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango vya juu zikiwamo Dar City, Stein Warriors, Pazi, JKT, UDSM Outsiders, Srelio na ABC.

Savio iliwahi kuwa bingwa wa ligi hiyo mwaka 2016, 2017, 2018 na 2021 kabla ya kupoteza makali na kwa sasa inasubiri msimu mpya wa BDL utakaotangaza baada ya mabosi wa BD kukutana.