MADIWANI KIBAHA WAFANYA ZIARA YA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KATA 4

 

…………………

Waheshimiwa Madiwani wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira pamoja na Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii za Manispaa ya Kibaha wamefanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata 4 za Manispaa hiyo.

Ziara hiyo iliongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Ginhu Nicas, ambapo Madiwani hao walitembelea na kukagua Mradi wa Dampo la Misugusugu, Ofisi za Taasisi zilizopimwa na kupewa hati, Zahanati ya Misugusugu, Ofisi ya Kata ya Visiga pamoja na Shule ya Msingi Maili 35.

Aidha, kamati hizo pia zilikagua miradi ya ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Mwalimu Nyerere Kata ya Sofu, pamoja na Shule ya Awali na Msingi Mwambisi, miradi ambayo ipo katika Kata ya Kongowe.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Ginhu Nicas, amesema kuwa kamati hizo zimeridhishwa na utekelezaji wa miradi yote waliyoikagua, na kupongeza juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, pamoja na timu ya wataalamu kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.

“Tumejionea kazi nzuri iliyosimamiwa kwa weledi mkubwa. Hakika Manispaa imepiga hatua kubwa ya maendeleo, ikiwemo kupima maeneo ya taasisi na kuyapatia hati, jambo linaloimarisha usalama wa mali za umma na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Dkt. Nicas.

Ameongeza kuwa Manispaa itaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa viwango vinavyokubalika na kuwanufaisha wananchi wa Manispaa ya Kibaha.