Mahakama ilivyoibana Serikali shauri la Mwambe, familia kunyang’anywa pasipoti

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeipa Serikali siku mbili badala ya 14 ambazo iliziomba, kujibu madai ya waziri wa zamani, Geofrey Mwambe, katika shauri lake la kunyang’anywa hati za kusafiria, yeye na familia yake.

Mwambe ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mbunge wa Masasi, Mtwara (CCM), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara anadai kunyang’anywa hati zake za kusafiria yeye familia yake na kuzuiliwa kusafiri nje ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, amefungua shauri la mapitio ya mahakama dhidi ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiomba mahakama imruhusu kufungua shauri la mapitio ya mahakama ili mahakama hiyo imuamuru Kamishana wa Uhamiaji kuachia na kukabidhi hati zao hizo.

Mwambe kupitia mawakili wake Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura akidai hati hizo zinashikiliwa na Kamishna wa Uhamiaji kinyume cha sheria na bila msingi wowote wa kisheria.

Katika hati hiyo ya dharura, mawakili Mpoki na Mwasipu wanathibitisha udharura wa shauri hilo wakidai kuwa  usikilizwaji wake ni wa dharura ya hali ya juu sana kwa sababu, kwanza mwombaji, Mwambe ni mgonjwa na anatakiwa kusafiri kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo wanadai kuwa hawezi kusafiri kwa kuwa hati zake za kusafiria pamoja na za mke wake ambaye atasafiri naye kwa ajili ya kumhudumia kwa karibu, zimekamatwa na mjibu maombi wa kwanza, Kamishna wa Uhamiaji.

Hivyo wanadai kama maombi hayo hayatatasikilizwa kwa dharura, hali yake ya afya itaendelea kudorora na kusababisha madhara makubwa kwake.

Shauri hilo lililopanga kusikilizwa na Jaji David Ngunyale limetajwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza leo, Jumanne, Januari 20, 2026, mbele ya Naibu Msajili, Livin Lyakinana.

Wakati lilipoitwa mahakamani, wakili Mpoki ameieleza mahakama shauri hilo linaitwa kwa mara ya kwanza na kwamba limepangwa kwa Jaji Ngunyale.

“Tumeambiwa kuwa hayupo (jaji), hivyo tunaomba wajibu maombi wawasilishe majibu yao na kiapo kinzani ili shauri liendelee kwa tarehe ambayo jaji atakuwepo,” amesema Wakili Mpoki.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daniel Nyakiha ameieleza mahakama kuwa walipewa nyaraka za shauri hilo jana muda ukiwa umeshakwenda na akaomba siku 14 za wajibu maombi kuwasilisha majibu yao dhidi ya maombi hayo pamoja na kiapo kinzani.

Akijibu swali la Naibu Msajili Lyakinana kwa kuwa shauri hilo limefunguliwa kwa hati ya dharura ni kwa nini siku hizo zisipunguzwe zikawa mbili, wakili Nyakiha amesema kuwa kwa kuwa shauri hilo linaihusisha Uhamiaji.

Amesema hivyo wanawajibika kuwatafuta maofisa Uhamiaji kupata maelezo yao na kwamba katika mazingira hayo siku mbili itakuwa vigumu kwa kuwa watakuwa hawajapata cha kujibu.

Hata hivyo Naibu Msajili Lyakinana baada ya kuwasiliana na Jjai Ngunyale kujua ratiba yake, ameipa Serikali siku mbili kuwasilisha majibu yake pamoja na kiapo kinzani, huku akipanga shauri hili lisikilizwe Ijumaa, Januari 23, 2026.

‎”Kwa kuwa shauri hili limefunguliwa chini ya hati ya dharura, wajibu maombi watawasilisha majibu yao pamoja na kiapo kinzani ndani ya siku mbili na shauri hili litasikilizwa Ijumaa, Januari 23, 2026 saa 4:00, amesema Naibu Msajili Lyakinana.

Hati ya maombi ya shauri hilo inaungwa mkono na kiapo cha Mwambe mwenyewe na kiapo cha mdogo wake, Nestory Chilumba, ambapo anasimulia namna alivyonyang’anywa hati zake za kusafiria na za familia yake wakiwa safarini kuelekea Nairobu Kenye na kisha Ujerumani.

Kwa mujibu wa kiapo chake, Mwambe ambaye ni Mtanzania na mmiliki wa hati ya kusafiria namba TDE011349 na mkewe Tumaini Jason Kyando anamiliki hati ya kusafiria namba TAE181501.

Katika ndoa yao wamebarikiwa kupata watoto watatu ambao bado ni wadogo, Kinkil Geoffrey Mwambe, anayemiliki hati ya kusafiria namba TAE923387; Karen-pracht Geoffrey Mwambe, mwenye hati namba TAE925212 na Kathrin-lena Geoffrey Mwambe, mwenye hati namba TAE903654.

Desemba 17, 2025, alisafarini kuelekea Ujerumani kupitia Kenya kwa ajili ya matibabu.

Katika Kituo cha Mpaka cha Namanga, aliwasilisha hati zake za kusafiria kwa madhumuni ya kupata muhuri wa kutoka Tanzania ili apate muhuri wa kuingia Kenya na kuendelea na safari yake Ujerumani kwa matibabu.

Alichagua kutumia njia ya Kenya kwa kuwa taratibu za kupata Visa ya Schengen ni rahisi, za haraka na zenye ufanisi zaidi ikilinganishwa na taratibu zilizopo Dar es Salaam ambazo huchukua muda mrefu zaidi.

Pia mke wake na watoto wao watatu walitarajiwa kusafiri kupitia cha mpaka wa Sirari wilayani Musoma, kwa nia ya kwenda likizo za Krismasi katika Hifadhi ya Taifa ya Masai Mara na baadaye kuungana naye Nairobi kwa ajili ya maombi ya Visa ya Schengen.

Hivyo siku hiyo alimkabidhi hati yake ofisa Uhamiaji mmoja aitwaye Patrick Mkande, na baada ya muda mfupi, ofisa huyo alimwambia kuwa hati yake inaonesha kuwa yeye ni mtumishi wa umma na hivyo anahitaji kibali cha mwajiri kusafiri nje ya nchi;

Mwambe alikataa kuwa kwa sasa si mtumishi wa umma tena (Mbunge) na ofisa huyo alimuomba. asubiri ili awasiliane na mkuu wake juu ya tofauti ya hadhi iliyoonekana kwenye hati yake kutoka kuwa mtumishi wa umma hadi raia wa kawaida, kwa kuwa watumishi wa umma huhitaji kibali cha kusafiri.

Iilichukua zaidi ya saa saba na ofisa huyo alimweleza kuwa mpaka muda jhuo hakuna jambo lolote lililokuwa limefanyika kuhusu uhakiki wa hati hiyo.

Hivyo Mwambe alilazimika kuamua kurudi Dar es Salaam kwa kuwa kuendelea kubaki Namanga katika hali yake ya ugonjwa kulikuwa na madhara kwa afya yangu.

Alipomuomba ofisa huyo amrudishie hati yake ili arudi Dar es Salaam na kupata ufafanuzi zaidi na maofisa wa Uhamiaji kuhusu hadhi ya hati yake, lakini afisa huyo alikataa.

Hali kama hiyo hiyo iliwakuta mkewe na watoto wao watatu waliokuwa wakivuka katika kituo cha mpaka cha Sirari, ambapo pasipoti zao zilikamatwa na maofisa wa Uhamiaji, nao wakaamua kurudi Dar es Salaam.

Alipowasili Dar es Salaam akiwa mgonjwa, aliwaomba wakili wake Hekima Mwasipu na mdogo wake Nestory Chilumba waende kuchukua pasipoti zake pamoja na za mkewe na za watoto wao kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji katika ofisi yake ya Kurasini.

Wakili na mdogo wake walikutana na Kamishna wa Uhamiaji ofisini kwake Desemba 24, 2025, Kamishna baada ya kuwasiliana na maofisa wa Uhamiaji katika vituo husika vya mipakani, walimweleza kuwa pasipoti hizo zilichukuliwa na maafisa hao katika vituo hivyo.

Pia, Kamishna aliwaeleza kuwa alikuwa akifanyia kazi suala hilo kubaini sababu za kukamatwa na kuchukuliwa kwa hati hizo, lakini mpaka anaapa kiapo hicho kufungua shauri hilo, Kamishna alikuwa hajamjibu wala kumpa sababu zozote za kukamatwa na kuchukuliwa kwa hati zao.

Aliwaelekeza mawakili wake hao, Mpoki na Mwasipu kutoa barua rasmi ya madai ya siku tatu kwa Kamishna wakimtaka arudishe hati zao au atoe hati mpya badala yake.

Hata hivyo licha ya barua hiyo Kamishna hajatimiza madai hayo ya kurejesha hati hizo wala kutoa mpya badala yake hadi sasa.

Mwambe anadai kuwa kwa maelezo hayo aliyoyatoa Kamishna hana haki yoyote ya kisheria ya kuendelea kushikilia hati hizo, na ana wajibu wa kisheria kurejesha hati hizo, kwa kuwa ni haki yake kuendelea kuwa nazo hadi zitakapokwisha muda wake wa matumizi.

Anafafanua kamishna hajawahi kutoa sababu yoyote inayoonesha kuwa si halali yeye kuwa na hati hizo za kusafiria; na hata kama ingekuwa hivyo, ilikuwa ni kosa kwake kuchukua hatua hizo bila kuwapa wamiliki wa hati hizo haki ya kusikilizwa.

Anasisitiza kitendo cha kukamata na kuendelea kuhifadhi hati hizo za kusafiria kinyume cha sheria kimemnyima haki yake ya Kikatiba ya uhuru wa kusafiri, kama inavyolindwa chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa mara kwa mara.

Anaongeza kuwa kitendo hicho ni batili kisheria na kinakiuka misingi ya haki asilia,

“Hivyo, kwa heshima na unyenyekevu ninaomba Mahakama iridhie kutoa ruhusa ya kufungua maombi ya mapitio ya kimahakama,” amehitimisha Mwambe.

Amesema kuwa anaoma ruhusa hiyo ya mahakama ili afungue shauri la mapitio ya mahakama ili itoe amri ya kumlazimisha Kamishna wa Uhamiaji kuachilia  na kukabidhi hati zao hizo kama zilivyotajwa.

Desemba 7, 2025, Mwambe alitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi katika makazi yake eneo la Tegeta, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, usiku na baadaye alihojiwa kwa tuhuma za kula njama za kutaka kumuua Mkuu wa Polisi na uchochezi wa kimtandao.

Aliachiliwa Desemba 15, 2025 siku ambayo shauri lake la maombi ya kutaka afikishwe mahakamani lilikuwa limepangwa kusikilizwa.