Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amekutana na kufanya mazungumzo na rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Gianni Infantino katika ofisi za FIFA zilizopo Jijini Rabat, nchini Morocco.
Katika mazungumzo hayo Makonda amemshukuru Infantino kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Tanzania katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na amemhakikishia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza inaunga mkono jitihada hizo na ipo tayari kushirikiana na FIFA.
Amemueleza Infantino kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kuchangia katika maendeleo ya mpira wa miguu vikiwemo vipaji vya vijana wengi, maeneo ya kujenga miundombinu ya michezo na utashi wa kisiasa, na kwamba FIFA inakaribishwa kushirikiana na Serikali katika uwekezaji huo.
Aidha, Makonda amemkaribisha rais huyo na amemwambia Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa matukio mbalimbali ya FIFA ikiwemo mashindano, mikutano na ziara za viongozi na wataalamu.
Kwa upande Infantino amemshukuru Makonda na ujumbe wake kwa kumtembelea na amesema FIFA ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika programu zake za maendeleo ambazo zitasaidia kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na mchezo wa mpira wa miguu ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uendelezaji wa vituo vya ufundi.
Infantino ameipongeza Tanzania kwa kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Serikali ya ujenzi wa miundombinu ya michezo kuelekea AFCON 2027 na amesema FIFA inaunga mkono jitihada hizo.
Katika mazungumzo hayo Makonda aliongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, Balozi wa Tanzania nchini Morocco, Ali Mwadini, rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo Boniface Tamba na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Neema Msitha.