Lushoto. Wananchi wa kata ya Lunguza katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamelalamikia uwepo wa makundi makubwa ya tembo ambayo yamekuwa yakiharibu mazao mashambani, kuharibu miundombinu ya maji na wakati mwingine kusababisha vifo vya watu, hali inayowafanya kuishi kwa hofu.
Wakizungumza na Mwananchi Januari 20, 2026, wananchi hao waliiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kwa kuyafukuza makundi hayo ya tembo kutoka kwenye makazi yao na kuyarejesha kwenye hifadhi, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo na ufugaji bila vitisho.
Mkazi wa kijiji cha Kiwanja, kata ya Mnazi wilayani Lushoto, Kingazi Ally, amesema tembo wamekuwa wakifukia mabwawa waliyoyachimba kwa ajili ya maji ya kunywa na mifugo, hali inayosababisha adha kubwa kwa jamii ya wafugaji.
“Mpaka sasa tunafikiria kuchimba tena mabwawa, lakini haitasaidia kwa sababu mara tu baada ya kuchimba tembo wanahamia hapo na kuanza kufanya uharibifu. Mbali na mazao kuharibiwa, watu pia wanauawa. Ukisikia habari kutoka vijiji vya pembezoni, ni vifo na uharibifu wa mashamba,” amesema Ally.
Ally ameongeza kuwa hivi karibuni katika kijiji cha Lunguza, mtu mmoja aliuawa na tembo, hali iliyosababisha hata watoto kushindwa kwenda shule kwa hofu ya kuvamiwa.
“Hata kwenda sokoni imekuwa shida. Tunaomba hawa tembo wafukuzwe warudishwe kwenye hifadhi. Kama wananchi tumeshindwa, tunamuomba Rais mwenyewe aingilie kati,” amesema.
Kwa upande wake, Matachu Ligase amesema watoto wao wanapata shida kubwa kutokana na uwepo wa tembo, huku baadhi wakishindwa kuhudhuria masomo kwa hofu ya kukutana na makundi hayo.
Amesema hali hiyo inaweza kuathiri maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao.
Mkuu wa Wilaya la Lushoto Mkoani Tanga Zephania Sumaye akizungumza na vyombo vya habari juu ya hatua zinazochukuliwa kukabilia na Tembo Tarafa ya Umba katika wilaya hiyo.
Ligase ameongeza kuwa kukaa kwa muda mrefu kwa tembo kwenye makazi ya watu kunawafanya wananchi washindwe kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, hususan kilimo na ufugaji, ambazo ndizo tegemeo lao kuu la maisha.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kiwanja Omari Mwanfula amesema wananchi wa kijiji hicho wanakabiliwa na hatari ya njaa kutokana na tembo kuvamia mashamba na kuharibu mazao.
Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuhakikisha wananchi waliopata madhara wanalipwa fidia kwa wakati ili kupunguza ugumu wa maisha yao.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilaya ya Lushoto, Zakayo Ngioko, amesema tembo wamekuwa kikwazo kikubwa kwa jamii ya wafugaji na wakulima, hali inayosababisha mauaji na kuongeza hofu kwa wananchi.
“Hivi karibuni tulipata taarifa ya mzee mmoja wa Kimang’ati aitwaye Robert, mkazi wa kijiji cha Lunguza, aliyeshambuliwa na tembo na kisha kuuawa. Kwa kweli tembo wamezidi, hofu imeongezeka kwa wachungaji, wakulima na wanafunzi,” amesema Ngioko.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, amesema jitihada zinaendelea kuhakikisha tembo wanaondolewa kwenye makazi ya watu na kurejeshwa kwenye hifadhi ili wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida.
“Tarafa ya Umba kwa ujumla ina changamoto ya tembo wanaotoka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi. Hali ya ukame iliyozidi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kenya, imesababisha tembo kutoka pori la Tsavo kuvuka mpaka na kuingia kwenye makazi ya watu,” amesema Sumaye.
Sumaye ameipongeza Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Tawa) kwa jitihada zao za kudhibiti tembo kwenye makazi ya watu, akisema wamefanya kazi kubwa lakini changamoto bado ipo.
Ameongeza kuwa eneo hilo lipo kwenye korido za wanyamapori, na tembo huwa hawasahau mapito yao ya asili. “Tumezungumza na wataalamu wa maliasili na tumefanikiwa kuwafunga kola tembo katika makundi makubwa matatu kwa Lushoto , Korogwe Mkinga, ili kuwafuatilia wanapotoka hifadhi na kuingia kwenye makazi ya watu,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha wananchi wa maeneo yaliyoathiriwa wanaendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila hofu, huku tembo wakidhibitiwa kwa njia endelevu.