Mambo magumu Simba, kocha agusia mawili

KOCHA wa Simba, Steve Barker amekiri wazi kuwa na kibarua kigumu cha kufanya kutokana na kiwango cha timu hiyo, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, huku akigusia mambo mawili ambayo ni kuboresha utimamu wa wachezaji na kukamilisha haraka mchakato wa usajili.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Barker katika Ligi Kuu Bara tangu aanze kuifundisha Simba huku ikiwa ya sita kwa timu hiyo ambayo imefikisha pointi 13 ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, nyuma ya Pamba Jiji (16), Yanga (16) ambayo jana ilikuwa uwanjani kucheza dhidi ya Mashujaa na JKT Tanzania yenye pointi 17.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker, amesema: “Tulianza mchezo kwa nguvu na kuwa na umiliki mkubwa wa mpira, kitu kilichokuwa muhimu kwetu tulitakiwa kupata bao la pili baada ya kupata bao la kwanza, tulikuwa na nafasi nyingi nzuri za wazi kufunga, lakini haikuwa hivyo na mwishowe wakasawazisha.”

Kocha huyo alielezea, hali hiyo ilitokana na baadhi ya maamuzi yasiyo sahihi.

“Baada ya kufungwa bao, tulijaribu kuanzisha mashambulizi zaidi, lakini hatukufanikisha kutokana na maamuzi yasiyo sahihi. Kila mchezaji anatakiwa kuboresha kiwango chake na timu kwa jumla inahitaji kuimarisha hali ya upambanaji,” amebainisha.

SIMB 01


Kocha huyo aliendelea kusema: “Kutokuwepo kwa baadhi ya wachezaji kunatuathiri, pia kunatoa nafasi kwa wengine kuonyesha uwezo wao. Tumekuwa na mchakato wa usajili na nina imani wachezaji wapya watakamilisha mchakato huu siku chache zijazo.”

Barker pia aligusia umuhimu wa kuimarisha utimamu wa wachezaji wake kimwili kwa kusema: “Kuna baadhi ya michezo yetu inayohitaji viwango bora zaidi vya utimamu wa mwili, wachezaji watatakiwa kujitoa zaidi kwa dakika zote 90.

SIMB 03


“Tunaendelea kufanya kazi kwa muda ambao upo mbele yetu ili kuboresha hali ya kisaikolojia kwa wachezaji na kimfumo ya timu, ili kila mchezaji aweze kutoa kiwango cha juu katika kila mechi.”

Kocha Barker aliweka wazi kuwa, mechi za kimataifa zinazokuja, ikiwemo dhidi ya Esperance ya Tunisia itakayochezwa Jumamosi wiki hii ugenini, zitakuwa na changamoto kubwa.

SIMB 02


“Tunahitaji kuhakikisha timu iko katika hali bora zaidi kwa mechi za kimataifa. Hatuwezi kuruhusu kucheza kama tulivyofanya dhidi ya Mtibwa Sugar. Kila kitu ni mchakato na kazi inaendelea,” amesema.

SIMB 04


Aidha, Barker alieleza nafasi za wachezaji wapya ni muhimu katika kuimarisha kikosi cha Simba akiamini siku chache zijazo wataimarika kiuchezaji.

“Wachezaji wapya wanapaswa kuchukua nafasi zao kikamilifu. Hii ni nafasi ya kuonyesha uwezo na nina imani kuwa katika siku chache zijazo tutakuwa na timu yenye nguvu zaidi,” amesema.

Kocha huyo pia alibainisha maeneo ambayo yanahitaji kuimarishwa, ikiwemo nafasi ya golikipa kutokana na jeraha la muda mrefu la Moussa Camara pamoja na Yakoub Suleiman.